Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nabi meno yote nje

Dee81fbd526296215cba07a3cf5f7432 Nabi meno yote nje

Mon, 4 Oct 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KOCHA ya Yanga, Nasriddine Nabi amesema anafurahi kuona timu yake ikiendelea kuimarika siku baada ya siku licha ya kupata ushindi mwembamba kwenye mechi mbili za Ligi Kuu Tanzania Bara walizocheza hivi karibuni.

Yanga ilipata ushindi wake wa pili juzi kwa kuifunga Geita Gold bao 1-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam na kujikita katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi nyuma ya vinara Polisi Tanzania, zote zikiwa na pointi sita zikitofautiana kwa mabao ya kufunga.

Akizungumza baada ya mchezo dhidi ya Geita FC, Nabi alisema inaridhisha kuona timu ikizidi kuimarika katika kila mechi walizocheza na hiyo inampa matumaini ya kufanya vizuri zaidi kwenye ligi hiyo.

“Niwapongeze wachezaji kwa ushindi wa pili mfululizo kwenye ligi, mchezo ulikuwa mzuri kwa timu zote mbili lakini tulistahili kupata ushindi kutokana na kiwango ambacho tulikionesha, tumeonesha ubora halisi wa timu nitakayokuwa nayo msimu huu,” alisema Nabi.

Kocha huyo raia wa Tunisia alisema anapambana kuongeza utimamu wa mwili pamoja na umaliziaji kwa wachezaji wake kwani imekuwa tatizo katika mechi walizocheza.

Alisema wakati wa mapumziko mafupi ya ligi kwenye kambi ya muda mfupi watakayoweka mkoani Arusha, anaamini itampa nafasi kurekebisha kasoro zote.

“Tunatarajia kwenda Arusha kwa mapumziko mafupi baada ya ligi kusimama kupisha maandalizi ya timu za taifa kuwania kufuzu Kombe la Dunia la Qatar 2022, tukiwa Arusha tutarekebisha mapungufu ikiwamo suala la umaliziaji na timu kuishiwa pumzi kipindi cha pili,” alisema.

Kwa upande wake, Kocha Msaidizi wa Geita FC, Fredy Felix Minziro alisema kupoteza mchezo huo kulitokana na wachezaji kuanza mchezo chini wakiwahofia wapinzani wao, lakini kadri muda ulivyokwenda walirudi mchezoni na kama washambuliaji wangekuwa makini wangepata angalau pointi moja.

Chanzo: www.habarileo.co.tz