Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nabi ataka makali zaidi Yanga

A0d5f90bf1c60ef82f41b86b76b86fb8.jpeg Nabi ataka makali zaidi Yanga

Thu, 4 Nov 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KOCHA Mkuu wa Yanga Nasriddine Nabi, amesema pamoja na ushindi mnono walioupata dhidi ya Ruvu Shooting, bado timu hiyo ipo katika kipindi cha mpito kuelekea kwenye ubora anaouhitaji.

Yanga juzi iliandikisha ushindi wake wa tano mfululizo kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara, kwa kuifunga Ruvu Shooting ya Pwani mabao 3-1, katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Nabi alisema juzi kuwa anafurahi kuona kile alichoahidi cha kupewa muda wa kuitengeneza timu hiyo kimeanza kuonesha matunda kwa ushindi wanaoupata, lakini bado ana kiu ya kuijenga zaidi timu hiyo.

“Nafurahi kuona tunacheza na kupata ushindi kwenye mechi zetu tano za ligi mchezo wa leo (juzi), ulikuwa mgumu. Ruvu ni timu nzuri siku zote huwa inajiandaa kucheza na timu kubwa, msimu uliopita tuliwafunga kwa tabu mabao 3-2, lakini pia waliifunga Simba bao 1-0, siyo wa kuwadharau,” alisema.

Kocha huyo raia wa Tunisia alisema matokeo wanayoyapata hivi sasa ni sehemu ya kile alichokiahidi wakati anakuja nchini kwamba anataka kutengeneza utambulisho halisi wa Yanga (DNA), kwa sababu ya ukubwa iliyonayo timu hiyo Afrika Mashariki.

Alisema ingawa watu wameanza kuwafananisha na FC Barcelona kwa aina ya soka la pasi nyingi wanalocheza, lakini hakuna ukweli katika hilo, kwani Yanga itabaki kama Yanga kwa kucheza soka la aina anayotaka yeye hivi sasa.

“Ninachotaka siyo kumfunga mpinzani mabao mengi, lakini pia tucheze soka la kuvutia lenye pasi nyingi lionekane kwa mashabiki, ambao wanajazana kwa wingi kuja kutupa sapoti na hilo linawezekana kwa mwenendo tuliokuwa nao, hivyo ikitimia miezi mitatu niliyoahidi watu watajionea,” alisema Nabi.

Kwa upande wake, kocha wa Ruvu Shooting, Boniface Mkwasa alisema sababu ya timu yake kupoteza mchezo huo ilikuwa ni mwamuzi, Emmanuel Mwandembwa aliyekuwa na maamuzi ya utata katika baadhi ya matukio, ikiwemo penalti ambayo ilizaa bao la pili la Yanga.

Mkwasa alisema ukitoa kasoro hizo mchezo ulikuwa mzuri na aliwapongeza Yanga kwa ushindi walioupata na hiyo ilitokana na ubora walionao hivi sasa ambao ulisababisha wachezaji wake kufanya makosa mengi na wao kuyatumia kufunga mabao hayo.

Wakati huohuo, Coastal Union ya Tanga jana ilishindwa kutamba kwenye Uwanja wao wa nyumbani wa Mkwakwani, baada ya kulazimishwa suhulu dhidi ya Tanzania Prisons.

Chanzo: www.habarileo.co.tz