Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NBA imesafisha macho yangu ili nisimulie Watanzania

Mon, 27 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Katika safari isiyokuwa ndefu takribani saa nne na nusu kutokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, nilitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver R. Tambo katika jiji la Johannesburg, Afrika Kusini.

Nilishuka kwa ajili ya kushuhudia na kutoa habari juu ya tukio kubwa la NBA Africa ambalo uhusisha wachezaji wa mpira wa kikapu Ligi ya NBA wenye asili ya Afrika wanaocheza dhidi ya wachezaji waliopo kwenye NBA kutoka katika mataifa mengine.

Kimsingi NBA wanatumia nafasi hii kusaka vipaji, kueneza jina lao kwa maana ya masoko na mahusiano ya umma na mwisho kuendelea kuvutia wawekezaji wengine kwenye miradi yao.

Safari yangu ilikuwa inahusu kazi yangu ya uandishi wa habari lakini ndani ya moyo wangu nilikwenda kujifunza mengi zaidi kuhusu namna wenzetu wanavyojua kuandaa mashindano, tafrija na matukio yao kwa ujumla.

NBA wanafahamu fika kuwa michezo yao mingi Afrika wengi hatutazami kwa sababu ya tofauti ya muda dhidi ya Marekani ambako michezo hii inafanyika hivyo suala la msingi kwao ni kufikia adhira hii ambayo ni kama imejitenga.

Katika kusafisha yangu macho, nimeshuhudia mashindano ya vijana chini ya umri wa miaka 17 yanayoendelea hapa hadi michezo mikubwa inayoandaliwa kwenye soka.

Kama haitoshi, mashindano ya kikapu kuanzia ligi za ndani mpaka michuano ya kimataifa tunayoandaa, na mashindano mengine kama gofu, mpira wa pete, riadha na mingine mingine.

Ukiacha ukubwa wa NBA AFRICA GAME ambayo huuza tiketi zote, huwezi kukuta mechi ya upinzani kati ya Kaizer Chiefs na Orlando Pirates ina ukawaida wa Simba na Yanga. Maandalizi ni ndani na nje ya uwanja kibiashara na wananchi wa Afrika Kusini wameshaaminishiwa kuwa matukio kama haya ni matukio ya kipekee na wanatakiwa kuyakumbatia kwani mara chache hutokea.

Unapotua uwanja wa ndege tu O.R Tambo, unapata hisia za tukio lililokuwepo hapo, watu wa PR na Masoko wanafahamu kazi yao. Uwanja umependeza na mabango, matangazo ya video ya mchezo huo na maelekezo ya mfululizo wa matukio pamoja na majina ya wachezaji mpaka wasanii watakaohusika kisha namna ya wewe kununua tiketi.

Hali hii unaikuta pia kwenye maeneo mengi yenye watu wengi kama Mlimani City zao, Kariakoo zao, Posta zao, vituo vya treni (ambayo kwetu ni vituo vya daladala) na kwenye maeneo mengine mengi. Ukiachana na hilo, kuna kazi kubwa inafanywa ya kuhakikisha matukio haya yana wadhamini (partners) wengi ambao wanatoa fedha nyingi ya kawaida na sio mdhamini mmoja ategemewe kutoa fedha yote.

Hii inatoa nafasi ya kukusanya mapato mengi zaidi lakini kila mdhamini anakuwa amewekewa eneo ambalo anaweza kupata thamani yake na kuonekana kwa chapa yake vyema. Kwenye hili ndio utakuta wiki ya NBA AFRICA GAME inaanzia kwenye kusaka vipaji kupitia vijana kutoka mataifa zaidi ya 30 inayoitwa basketball without borders.

Kwa Tanzania tulikuwa na vijana wawili Jessica Ngisayise na Atiki wakiwa na kocha wao ndugu Bahati Mgunda. Thamani ya kwanza anayopata mdhamini (NIKE) ni vijana hawa wakiwa mafunzoni kutumia vifaa alivyozalisha yeye tu na hakuna ingizo la vifaa vingine. Hapa kimsingi wanakuwa wanafahamu fika namna ambayo kwa wiki nzima watajenga hisia na fikra kichwani kwa hawa vijana takribani 160 kuwa hawa ndo wazalishaji bora wa jezi na viatu.

Lakini pia mashirika ya ndege yanayokuwa yameingia mkataba na NBA yanakuwa yanapewa haki ya kusafirisha vijana hawa. Nina uhakika ukienda leo kumuuliza mmojawapo wa vijana wa Tanzania hawa hawezi kutaja shirika lingine zuri la ndege la kwenda Afrika Kusini zaidi ya hilo lililowabeba. Hii ni thamani ambayo kwenye mashindano ya Tanzania hatujui kutengeneza.

Kisha inafika siku ya mchezo wenyewe ambayo wala hawapati watizamaji wengi kama wanaoweza kuingia uwanja wa Taifa kwa ajili ya mechi ya Simba na Yanga. Wao kwa Marekani watizamaji wao ni elfu ishirini mpaka thelathini na kwa Afrika kwenye mchezo huu huwa ni watizamaji elfu nane mpaka kumi ndo lengo lao.

Kwanini hawawazi viingilio? Sababu pekee ni kuwa tayari wametoa thamani kwa wawekezaji wengi na wameyapa mashindano ukubwa hali inayosababisha fedha ya kiingilio kutokuwa na hitaji lolote la msingi. Hili ni tukio la NBA ambapo kama unahisi ni maarufu unakuwa unajidanganya kwa sababu mchezo wa mpira wa kikapu kwa Afrika Kusini upo nyuma ya Soka, Cricket, na Rugby kwa umaarufu pengine hata na ndondi. Kinachowatofautisha wao na sisi ni jambo moja la ajabu nalo ni umakini katika utendaji kazi basi. Kila jambo lao wanalipa uzito, wanakupa sababu ya kuamini kuwa ni kubwa na la kipekee na kisha wanalipa thamani. Hawana jambo dogo hata kama ni kumpeleka mchezaji kuogelea baharini, watataka kukuthibitishia kuwa Yule mchezaji inabidi alipwe na bodi ya utalii kwa sababu anatangaza hilo eneo. Huu umakini sisi hatuna.

Nani alitudanganya kuwa mapato ya viingilio ndio chanzo kikuu cha mapato? NBA wametoka marekani wakaja kufanya balaa Afrika Kusini, wanaweza pia kuja Tanzania na wakafanya kubwa zaidi na hawayafahamu mazingira yetu lakini sisi hatuwezi. Umakini wetu upo chini mno. Nimesafisha macho, nimejifunza, nimefurahi na nimeona nizungumze na Watanzania kuhusiana na umakini na kufahamu namna ya kupangilia mipango yetu.

Chanzo: mwananchi.co.tz