Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NADIR HAROUB ‘CANNAVARO’ Beki aliyeacha alama Jangwani

11645 Pic+kanavaro TanzaniaWeb

Mon, 13 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wakati Yanga ikimuaga rasmi nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ aliyestaafu soka, pengo lake linaweza kuchukua muda mrefu kuzibika ndani ya klabu hiyo licha ya yeye mwenyewe kusema kuwa Abdallah Shaibu ‘Ninja’ kuwa anaweza kuziba pengo lake.

Mafanikio aliyopata Yanga, nidhamu ya maisha nje, ndani ya uwanja na uhusiano uzuri baina yake na wachezaji wenzake ni miongoni mwa sifa zinazombeba Cannavaro.

Pia uhusiano wake na benchi la ufundi, viongozi na wadau wa soka nchini vinaonekana ni mfupa mgumu kwa wachezaji waliopo Yanga kufuata nyayo za beki huyo wa kati.

Wachezaji Kelvin Yondani, Juma Abdul, Andrew Vincent na Papy Tshishimbi mmoja ana nafasi ya kutangazwa nahodha mpya wa Yanga, yeyote kati yao atalazimika kufanya kazi kubwa kufikia daraja na hadhi aliyokuwa nayo Cannavaro.

Katika kipindi cha miaka 12 aliyocheza Yanga baada ya kujiunga nayo mwaka 2006 akitokea Malindi ya Zanzibar, Cannavaro ameshinda jumla ya mataji 15 yanayomfanya awe mchezaji mwenye mafanikio makubwa kuliko mwingine kwenye kikosi cha Yanga kuanzia mwaka 2000 hadi sasa.

Kama ilivyo kwa mchezaji mwingine wa Yanga muda mrefu miaka ya karibuni, Fred Mbuna, Cannavaro ameshinda mataji saba ya Ligi Kuu Tanzania Bara mwaka 2008, 2009, 2011, 2013, 2015, 2016 na 2017, mawili ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, manne ya Ngao ya Jamii na moja Kombe la FA.

Nguli huyo pia ameiongoza Yanga kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mara mbili mwaka 2016 na 2018.

Mafanikio hayo yalimfanya Cannavaro kupewa heshima kubwa Yanga kutoka kwa wachezaji, benchi la ufundi na mashabiki jambo ambalo lilimfanya awe na nguvu ya ushawishi katika uamuzi kwenye baadhi ya masuala muhimu.

Pamoja na staili yake ya kucheza soka la kutumia nguvu, Cannavaro ni miongoni mwa wachezaji ambao ilikuwa nadra kuadhibiwa kwa utovu wa nidhamu na mara kwa mara alionyeshwa kadi kwa rafu za kawaida mchezoni.

Beki huyo ndiye alikuwa kinara wa kuwatuliza wenzake wanapomzonga mwamuzi, mfano tukio la mwaka 2014 ambalo alifanya kazi kubwa kuwatuliza wachezaji walipotaka kumpiga mwamuzi Israel Nkongo katika mchezo dhidi ya Azam FC ambao Yanga ilipigwa mabao 3-1.

Ingawa Yondani anapewa nafasi ya kuwa nahodha atakayerithi mikoba, rekodi yake ya nidhamu haivutii na mara kwa mara amekuwa akijihusisha na vitendo visivyokuwa vya kiungwana uwanjani ambavyo vimekuwa vikichangia akutane na adhabu ya kufungiwa ama kupigwa kadi za mara kwa mara.

Upande mwingine ambao nahodha ajaye ana kibarua kigumu kufuata nyayo za Cannavaro ni uhusiano kwa vyombo vya habari, sifa ambayo nahodha huyo mstaafu wa Yanga imemtengenezea taswira nzuri kwa wadau wa soka nje na ndani ya nchi.

Akizungumza na gazeti hili, Cannavaro alisema anaamini Yanga itapata mtu sahihi wa kuziba nafasi yake na ametaja siri ya mafanikio yake kwa miaka 12 ndani ya klabu hiyo.

“Wachezaji wapo wazuri lakini kiukweli sifahamu nani anayeweza kuziba nafasi niliyoacha. Kikubwa niwaombe tu wachezaji wa Yanga wajitume, wawe na nidhamu na uvumilivu. Hiyo ndiyo siri ya mafanikio ambayo imenisaidia niweze kuichezea klabu kwa miaka 12 mfululizo.

Lakini pia nadhani tabia yangu ya kuheshimu mtu yeyote pasipo kuangalia mkubwa au mdogo nayo ni chachu ya mafanikio yangu.

Kingine ni kujitunza pindi wanapokuwa nje ya uwanja na kujiepusha na mambo yanayoweza kuhatarisha vipaji vyao kama vilevi, ngono na ulaji usiokuwa na mpangilio hasa vyakula vya mafuta,” alisema Cannavaro.

Beki huyo alisema kuwa hatasahau makali ya washambuliaji watatu waliokuwa wakimpa taabu uwanjani akiwemo nyota wa zamani wa Simba Haruna Moshi ‘Boban’.

“Nimekutana na washambuliaji wengi wazuri, lakini binafsi walionisumbua zaidi ni Samuel Eto’o wa Cameroon, Didier Drogba wa Ivory Coast na Haruna Moshi wa Simba,” alisema Cannavaro.

Alisema anajivunia kucheza pacha na Yondani, Salum Sued ‘Kusi’ akidai ni mabeki hodari ambao atawakumbuka katika kikosi cha Yanga.

Cannavaro alisema Yondani na Sued ni mabeki mahiri na hakuwa na presha walipounda safu ya ulinzi katika mechi husika.

Pia alimtaja beki wa Azam Aggrey Morris kuwa ni mmoja wa mabeki bora wa kati anayejivunia kucheza naye katika kikosi cha Taifa Stars.

Nahodha wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Ally Mayay alisema ingawa ni lazima Yanga iwe na nahodha mpya, hadhani kama Yondan ataweza kuvaa viatu vya Cannavaro.

“Uteuzi wa nahodha wa timu unalingana na utashi wa benchi la ufundi kwa kuangalia mchango wa mchezaji husika kikosini pamoja na uzoefu hivyo naona mtu kama Yondani anaweza kupata nafasi hiyo.

Lakini naona kabisa Cannavaro ameacha pengo kwa sababu ni mtu ambaye alikuwa na nguvu ya ushawishi na nidhamu iliyopitiliza, lakini kubwa zaidi ni utayari wake wa kujituma na kujifunza.

Cannavaro alikuwa na uwezo wa kuyabeba matatizo ya timu na kuyafikisha katika mahali sahihi pasipo kuathiri upande wowote ama wachezaji au uongozi. Na hii ni maana halisi ya nahodha kwamba unatakiwa ‘kubalansi’ mambo klabu inapopita katika kipindi kigumu,” anasema Mayay.

Chanzo: mwananchi.co.tz