Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwendo wa kushambulia tu

42102 Pic+watani Mwendo wa kushambulia tu

Mon, 18 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati watani wa jadi, Simba na Yanga wakikutana leo makocha wa timu zote mbili wamejilipua na kila mmoja kujinasibu kucheza soka la kushambulia.

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera na mwenzake wa Simba, Patrick Aussems wote wameahidi kuingia katika mchezo wa leo kwa kucheza soka la kushambulia hivyo kuonyesha mechi hiyo inaweza kuzalisha mabao mengi kama washambuliaji wa timu zote mbili watakuwa makini katika kufunga.

Kocha Zahera amepata tabasamu baada ya kurejea kwa mshambuliaji wame Amiss Tambwe aliyekosa michezo miwili iliyopita ya ligi baada ya kuwa na maumivu ya jicho na kushonwa nyuzi tano.

Tambwe amekuwa na rekodi nzuri dhidi ya Simba kwani ameifunga timu hiyo mara tatu mfululizo na aliwakosa msimu uliopita baada ya kuwa majeruhi wa muda mrefu wa goti.

Mshambuliaji huyo raia wa Burundi alianza kuwaonea Simba Septemba 26, 2015 Yanga iliposhinda mabao 2-0, bao moja akifunga Tambwe na lingine Malimi Busungu kisha akaifunga tena Simba Februari 20, 2016, Yanga iliposhinda mabao 2-0, bao lingine lilifungwa na Donald Ngoma halafu akaiongoza Yanga kutoka sare ya bao 1-1 Oktoba Mosi, 2016 na yeye akifunga bao moja.

Tambwe amesema wanachohitaji ni pointi tatu na anajua kuwa Simba imetoka kushinda mechi ya kimataifa lakini wasitarajie mteremko mechi ya leo.

“Wao wameshinda mechi ya kimataifa na sisi tumeshinda ya ligi hivyo mechi itakuwa ngumu kwani wote tunajuana. Kama nitafanikiwa kufunga nitafurahi kwani kazi ya mshambuliaji ni kufunga.

Simba pia inapaswa kuwa makini na Heritier Makambo ambaye anaongoza katika chati ya ufungaji bora wa Ligi Kuu Bara akiwa amefunga mabao 11. Licha ya kwamba kiwango chake katika mechi za karibuni kimeyumba kiasi cha kocha Zahera kumpa onyo lakini anaweza akaibuka kwenye mchezo wa leo na kufanya makubwa.

Pia mabeki wa Yanga itabidi wajipange kumzuia Emmanuel Okwi na Meddie Kagere ambao wako moto hivi sasa.

Okwi tangu ametua nchini ameshawahi kuifunga Yanga mabao matatu katika mechi mbili wakati Kagere bado hajaweza kutikisa nyavu za wapinzani wake hao licha ya kwamba ana mabao nane kwenye Ligi Kuu Bara.

Mei 6,2012 Okwi alifunga mabao mawili na kuiongoza Simba kuichapa Yanga mabao 5-0 kisha tena akaifunga Yanga Machi 8, 2015 , Simba iliposhinda bao 1-0.

Mpaka sasa Simba ina rekodi nzuri dhidi ya Yanga kwani iliifunga mechi nne kati ya saba za karibuni za mashindano yote. Januari 10, 2017, Kombe la Mapinduzi timu hizo zilitoka suluhu dakika 90 na Simba kushinda kwa penalti 4-2, Agosti 23 2017, Ngao ya Jamii timu zilitoka suluhu dakika 90 na Simba kushinda kwa penalti 5-4. Oktoba 28 mwaka huo huo kwenye Ligi Kuu Bara timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1, Aprili 29 mwaka jana kwenye Ligi Kuu Simba iliifunga Yanga bao 1-0 na Septemba 30 mwaka huo, zilitoka suluhu.



Chanzo: mwananchi.co.tz