Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwashiuya alivyojipanga msimu wa Ligi Kuu 2018/19

10352 Pic+mwashiuya

Mon, 6 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

“Mafanikio ya kitu chochote hayaji kirahisi”, hiyo ni kauli ya winga mpya wa Singida United, Geofrey Mwashiuya anayeamini kuondoka kwake Yanga sio mwisho wa ndoto yake ya kucheza soka nje ya nchi.

Mwashiuya angali anaikumbuka safari yake namna alivyotua Yanga, mwaka 2015 na kukiri kuwa hakutarajia kuvaa uzi wa klabu kongwe kama hiyo, yenye mashabiki lukuki akitokea timu ya Daraja la Kwanza, Kimondo FC ya Mbeya na kudai kama hiyo iliwezekana atashindwaje kucheza soka Ulaya ama kwingineko nje?.

Ameweza kufunguka mengi katika mahojiano maalumu na Spoti Mikiki kwamba kuachwa kwenye mpango wa kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera kwa msimu wa 2018/19, hakumaanishi kama ndio mwisho wa safari yake ya kisoka bali anachukulia kama changamoto ya safari anayoelekea katika kilele cha ndoto zake. “Kila kitu kina wakati wake, mfano wakati nacheza Kimondo nilikuwa natamani sana, nije nicheze timu moja na Salum Telela wakati yupo Yanga, nilivyomkuta tu, kwangu ilikuwa muujiza mkubwa sana, kama nilichoweza kuwaza mwanzo na kikawa nitashindwaje kufika ninapotaka,”anahoji.

MIAKA MITATU YANGA

Alijiunga na Yanga, mwaka 2015 akitokea Kimondo FC ya Mbeya, inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza, amekiri kuwa hiyo ilikuwa hatua kubwa ya maendeleo ya kazi yake ya soka, kitu kikubwa kuliko yote alichokipata hapo ni kwamba klabu hiyo imemtambulisha katika medani ya soka ndani na nje ya nchi.

“Yanga ni klabu kubwa, jina lake tu ni utajiri tosha, hivyo kuvaa jezi yao na kuitumikia kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, imenitambulisha na kulitangaza vilivyo jina langu.

“Kuna kipindi nilikuwa natafutwa sana na klabu za nje, naamini ipo siku moja ndoto hiyo itatimia, kwa sababu sijakata tamaa, naendelea kupambana ili kiwango changu kiwe juu,”anasema

Aliyekuwa kocha wa Yanga wakati huo, Hans Van Der Pluijm raia wa Uholanzi, aliyempokea Mwashiuya na kumpa nafasi aliwahi kukaririwa akisema kwamba, nyota huyo ni hazina kubwa kwa Taifa, endapo atajitambyua na kuwajibika ipasavyo kukiendeleza kipaji chake.

Kipindi hicho Pluijm alifananisha uwezo wa Mwashiuya na alivyokuwa Mrisho Ngassa ambaye alikuwa anatikisa ndani na nje ya nchi.

“Mwashiuya akizingatia kila anachoelekezwa atasikika anga nyingine, nimeona kitu katika mguu wake,” yalikuwa maneno ya Pluijm wakati huo.

SINGIDA UNITED

Anaitazama Singida United, kama kivuko cha kumpeleka ng’ambo kwa maana ya kucheza soka la nje ya mipaka ya Tanzania kama ilivyo kwa kina Simon Msuva anayecheza Difaa El Jadid ya Morocco, Mbwana Samatta aliyeko Genk ya Ubeligiji na Faridi Mussa aliyeko Getafe ya Hispania.

“Bado nina nafasi ya kucheza nje, ndio kwanza nina miaka 22, ninachotakiwa ni kujituma kwa bidii ili kuyaishi ninayoyakusudia, bila shaka nitafika hapo, njia ya kuyafikia ni kujituma na kutumia vema nafasi nitakayopata mbele ya kocha wangu mpya, Hemed Morocco,” anasema.

ANAVYOUONA MSIMU WA 2018/19

Anaitazama ligi ijayo yenye timu 20 kama itakayokuwa na ushindani wa hali ya juu, lakini kwake anaona ni kitu kizuri kitakachowapa wachezaji muda mwingi wa kutumika na kufanya wapate uzoefu mkubwa.

Chanzo: mwananchi.co.tz