Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwanariadha kutoka Filbert Bayi kusoma Marekani bure

441febc0bdc2ce652bb170ac062649fa.png Mwanariadha kutoka Filbert Bayi kusoma Marekani bure

Mon, 28 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MWANARIADHA chipukizi wa kimataifa wa Tanzania, Regina Mpigachai, amepata ofa ya kusomeshwa bure katika Chuo Kikuu cha Marekani cha Northern Colorado kwa gharama ya Sh milioni 80.

Regina ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Filbert Bayi iliyopo Kibaha, alikuwa akisomeshwa bure shuleni hapo kutokana na kipaji chake cha riadha, ambapo ameshiriki mashindano mbalimbali ya kitaifa na kimataifa kuanzia ya shule za msingi (Umitashumta), sekondari (Umisseta), Afrika na Olimpiki ya vijana.

Mwanariadha huyo anayekimbia mbio za mita 800 na 1500, anasoma kidato cha nne, ambapo pamoja na wanafunzi wengine zaidi ya 50 walishiriki mahafali ya kidato cha nne shuleni hapo juzi.

Akizngumza wakati wa kusaini mkataba na chuo hicho cha Colorado juzi, Mkuza, Kibaha, Mwenyekiti wa shule hizo, Filbert Bayi, alisema Regina amepata ofa hiyo kutokana na juhudi zake katika masomo na mchezo wa riadha.

Alisema kocha wa Chuo Kikuu cha Colorado alikuwa akifuatilia kwa karibu maendeleleo ya mwanariadha huyo tangu wakati wa Michezo ya Afrika nchini Morocco mwaka jana na katika mashindano ya taifa yaliyofanyika hivi karibuni, ambapo alifanya vizuri na kuuwezesha mkoa wa Pwani kutwaa ubingwa wa jumla.

Shule ya Filbert Bayi ilianza kumsomesha Regina shuleni hapo baada ya kubaini kipaji chake katika mashindano ya Umitashumta 2012 akitokea Shule ya Msingi Ndelema, mkoani Geita, katika kijiji cha Ndelema. Bayi alisema Regina atakuwa chuoni hapo kwa takribani miaka minne, ambapo atakuwa akisoma na kushiriki michezo na mbali na gharama hizo za masomo, chuo hicho pia kitakuwa kikimlipia gharama zote za safari zote za ndani na nje ya Marekani atakapoenda kushiriki mashindano mbalimbali.

Pia atakuwa akigharamiwa vifaa vya michezo, matibabu na huduma nyingine ambazo ni nje ya kiasi hicho cha fedha kilichotajwa. Kwa upande wa shule ya Filbert Bayi, imetumia Sh milioni 21 katika kipindi hicho cha miaka saba kumsomesha Regina.

Mama yake Regina ambaye alikuwapo katika hafla hiyo, Hellena John, aliushukuru uongozi wa FBS kwa kugundua kipaji cha mtoto wake na kukubali kumsomesha bure kwa kipindi chote na kumuwezesha kupata fursa ya kusoma nje Marekani, ambako pia ataendeleza kipaji chake.

Regina alisema hatawaangusha Watanzania kwani atakuwa balozi mzuri wakati wote atakapokuwa masomoni Marekani.

Alisema nidhamu kwake ndio itakuwa kitu cha kwanza na ataendelea kufanya juhudi katika masomo na mchezo.

Kocha wa mwanariadha huyo, Mmarekani Ron Davis, alisema hana wasiwasi na Regina kwani ana uhakika juhudi zake ataziendeleza na atafuata nyayo za Bayi, Suleiman Nyambui, Gidamis Shahanga na wanariadha wengine ambao walisoma Marekani enzi hizo.

Chanzo: habarileo.co.tz