Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwanangu kaokota makopo kajenga shule Msumbiji

Cheka Mszzzzzz Mwanangu kaokota makopo kajenga shule Msumbiji

Wed, 11 Sep 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Miaka sita imepita sasa tangu bondia wa ngumi za kulipwa nchini, Francis Cheka 'SMG' alipoachana na mchezo huo mwaka 2018 baada ya kutamba kwa miaka 18, kabla ya kutimkia zake Msumbuji ambako ni nchi ya asili ya mama yake mzazi, Maria Rafael.

Kwa miaka ya sasa, ni ngumu kusikia jina lake kama mengine yaliyozoeleka kwenye ngumi kama Twaha Kiduku, Karim Mandonga, Hassan Mwakinyo, Dullah Mbabe na Ibrahim Class hata hivyo sifa zake bado zinaishi.

Bondia huyo ambaye ni bingwa wa zamani wa Dunia wa mkanda wa WBF kuna wakati aliwahi kuitwa chizi kutokana na ajira yake nyingine ya kuokota makopo lakini hayakuacha kumpa heshima ya kipato kizuri cha fedha.

Kipindi akitesa ulingoni alicheza jumla ya mapambano 49, akishinda 34, kati ya hayo 18 ni kwa KnockOut na kupoteza 13 na kati ya hayo nane ni kwa KnockOut na amewahi kuambulia kutoa sare mbili pekee.

Katika nyakati zake za mwisho, Cheka hazikuwa nzuri kabisa kwani pambano lake la mwisho alipoteza kwa kichapo cha KnockOut ya raundi ya sita katika pambano la raundi 12 dhidi ya Dullah Mbabe, mwaka 2018 kwenye Ukumbi wa PTA.

Hadi anaachana na mchezo huo Cheka amesimama kwenye ulingo kwa kupigana raundi 328 ikiwa kila raundi moja ina wastani wa dakika tatu na jumla amepigana kwa dakika 984.

Mwanaspoti lilifika nyumbani kwa baba mzazi wa bondia huyo, mzee Boniface Cheka Sunguma, Kongowe Mzinga kwa lengo la kumjulia hali mzee huyu ambaye kwa muda mrefu amekuwa mlemavu wa macho na amekuwa sana na urafiki na mwandishi na licha ya tatizo hilo, amekuwa na ufahamu mkubwa wa kutunza kumbukumbu za watu mbalimbali wanaomtembelea kwa kutambua sauti zao huku akiwa mtu wa stori nyingi muda wote.

Hata hivyo, nikiwa nyumbani hapo, mzee Cheka alinitambulisha pia kwa mama wa Francis aliyeambatana na mwanaye huyo kuja kumjulia hali mzee wake wakitokea Msumbiji wanakoishi eneo la Mueda na kufanya naye mahojiano.

Ni raia wa msumbiji

Baada ya kujitambulisha majina yake 'Maria Rafael', lakini majina yake yanaonekana ni ya Kitanzania ila majibu yake yalisisitiza yeye ni raia wa Msumbiji.

"Haya ni majina yangu isipokuwa tofauti kubwa ipo katika utamkaji wake kwa sababu kule muda mwingi watu wanatumia lugha ya Kireno, inavyotamkwa lazima iwe tofauti.

Kumbe Cheka sio kama mabondia wengi. Msikie mama;

"Binafsi alikuwa ni mtoto wa kawaida kama walivyokuwa watoto wengine kwa sababu kila mtoto katika hatua za ukuaji anakuwa na tabia zake, wapo anaokuwa wakorofi kwa maana ya utundu na wengine wanakuwa wapole.

"Lakini kwa upande wake hakuwa mtu wa fujo sana ingawa kesi ndogondogo kwa watoto ni mambo ya kawaida hivyo hayakunipa shida kwake.

Cheka agoma kukaa Msumbiji, arejea Tanzania, ilikuaje?

"Nadhani ulikuwa utoto wake kwa sababu kule nilimwandikisha hadi shule lakini mwenyewe akaomba arudi Tanzania, hataki kusoma kule, nakumbuka yule kaka yangu wa Tanga alirudi naye.

Mama wala hajui Cheka kaibukaje kuwa bondia na alivyojua aliogopa, msikie;

"Kuhusu aliyemuibua na kipaji cheke, hata sijui hayo. Mimi na baba yake tulitengana akiwa na umri mdogo wakati huo tunaishi Kinondoni, ila nilienda kwa kaka yangu Tanga alikokuwa akiishi. Cheka nilimwacha kwa baba yake na hata nilipotoka Tanga, nilipita kwa baba yake nikamchukua, lakini nikamwambia narudi nyumbani Msumbiji baada ya kutengana kwetu."

"Kwanza hakuwahi kuniambia kabisa ila nilikuja kujua kutokana na matokeo ya mapambano, lakini kwa upande wangu sikufurahia kabisa yeye kuingia katika mchezo wa kupigana.

"Binafsi siku zote ngumi naona mchezo wa hatari kwa sababu wapo ambao tunasikia wanapata hadi vilema vya kudumu kwa sababu ya ngumi, sasa mwangu itakuaje."

Ushawahi kuangalia pambano lake lolote?

"Wakati wote wa yeye alivyokuwa anaenda kupigana sijawahi kuangalia kwenye runinga au kwenda ukumbini kuangalia kwa sababu nilikuwa sipendi yeye acheze kabisa ngumi ila nakumbuka safari moja alirudi kupigana akiwa na kidonda kikubwa usoni baada ya kupasuka.

"Nilivyomuona kiukweli nililia kwa sababu kama mzazi nilikuwa sipendi kabisa baada ya kuona hivyo, aliamua kuondoka nyumbani."

Upande wa familia yako Msumbiji walichukuliaje?

"Hakuna yeyote aliyekuwa anapenda, hasa wajomba zake maana kama kaka yangu mkubwa ambaye kwa Msumbiji ni mkuu wa Jeshi la Polisi IGP, Bernardino Rafael alikuwa akisema kabisa hapendi kumuona Cheka akicheza mchezo wa laana.

"Yeye alitamani sana kumwona katika mambo mengine ya kitaaluma hasa kama angesoma kule basi sasa hivi angekuwa kiongozi mkubwa Msumbiji, huenda jeshini au katika nafasi nyingine kutokana na ushawishi wa familia.

"Lakini alichagua kusoma huku akipoteza ingawa hakumaliza ikasababisha apoteze fursa zake nyingi ambazo pengine leo hii asingekuwa mtu wa huu mchezo wa ngumi kabisa.

Kuna waliomwita Cheka chizi kwa kuwa anaokota makopo, hata hivyo kwa mama yake anasifia mwanaye amepata bonge la dili.

"Nadhani hawakugundua alichokigundua yeye, ndiyo maana alikuwa akipewa hayo majina lakini kwake makopo yamempa mambo mengi kwa sababu hata sasa Msumbiji ndiye ameanzisha biashara ya kuokota chupa.

"Lakini siyo rahisi kwa watu kukubali lakini hayo makopo yamekuwa na faida kubwa kwa sababu hata ujio wetu huu ni kwa sababu ya tumekuja kuuza hayo katika viwanda vya hapa.

"Unajua amehamisha ile mashine yake ya Morogoro ambayo ilikuwa anaitumia kusaigia chupa sasa hivi ipo Mueda inafanya hiyo kazi ambayo inafanya analeta biashara yake huku.

"Sasa unamuita mtu chizi kwa sababu anaokota makopo lakini hayo makopo yamemfanya ajenge shule yake mwenyewe Msumbiji ambayo mpaka sasa imeshagharimu milioni 30 ingawa bado haijaisha.

Cheka anajenga shule?

"Ndiyo amekuwa akipambana sana kuhakisha ndoto yake ya kumiliki shule inafanikiwa na nimekuwa nikimpa sapoti katika usimamizi ili kukamilisha ambacho amekiwaza, nashukuru ujenzi upo katika hatua nzuri.

Ni shughuli za makopo peke yake anazofanya Msumbiji?

"Hapana amekuwa akifanya vitu vingi kwa sababu kule amekuwa mchimbaji wa madini katika migodi inayomilikia na familia na wakati mwengine pia huwa ananunua kwa ajili ya kuuza."

Ni kweli Cheka anakula vyura na konokono?

"Nadhani kwa nchi ya Msumbiji ni kawaida japokuwa upande wangu huwa situmii hivyo vyakula lakini Cheka yeye amekuwa akiwaandaa mwenyewe hao konokono au wakati mwengine vyura, nadhani kwake ni chakula cha kawaida."

Yupo mtoto wowote wa Cheka anayecheza ngumi?

"Sitamani kuona wajukuu zangu wacheze huo mchezo kabisa maana mpaka sasa watoto wake ni watano na hata yeye hataki wafanye hivyo, amekuwa akisema alicheza kwa sababu alikosa elimu sasa ataki watoto wacheze, amewawekea nguvu kubwa kwenye elimu.

Ajali ya moto wa Morogoro kuna watu walidai Cheka ni mmoja kati ya watu waliofariki dunia kutokana na ofisi yake kuwa karibu na eneo la tukio, ulipokeaje taarifa?

"Unajua wakati ule taarifa zake zinasambazwa amefariki dunia kwenye ile ajali ya moto, nilishtuka kwa sababu waliokuwa wakisambaza hawakuwa wakijua ukweli kwa sababu wakati huo Cheka alikuwa ameshaondoka Morogoro."

"Lakini naamini walikuwa wakisema kutokana na ukaribu wa eneo ambalo limetokea ajali na yeye kutoonekana ndiyo maana waliamua kuvumisha hivyo, ila mdogo wake Cosmas Cheka aliweka sawa taarifa kwa kukanusha juu ya jambo hilo."

"Sijui walifikiria kitu gani ila kwa kuwa mtoto wangu nilikuwa naye mwenyewe haikuweza kunipa shida sana kwa kuwa nilikuwa najua ukweli ulivyo."

Unategemea kumwona tena akipigana?

"Hapana sitarajii hilo jambo tena kwa sababu hata yeye aliniambia ukifika muda wake kuacha ngumi basi ataacha na ukweli tangu mwaka 2018 hajapigana tena.

"Lakini hata ukiangalia kwa hali, sasa yeye hawezi tena kurudi kupigana mambo yamebadilika anahitaji muda wa kutosha kuweza kusimamia shughuli zake mwenyewe," anasema mama Cheka.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live