Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwamuzi awatisha Simba mapema

39339 REFA+PIC Mwamuzi awatisha Simba mapema

Mon, 4 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

SIMBA imetua kibabe kule Misiri kwa ajili ya mechi yao dhidi ya Al Ahly, lakini kuna jambo ambalo limeanza kuwatisha mapema licha ya kuendelea kujenga moyo wa upambanaji na kusaka matokeo uwanjani.

Kikosi cha kocha Patrick Aussmes kimekutana na nuksi ya kupangwa kuchezeshwa na mwamuzi Maguette N’Diaye, ambaye hana rekodi nzuri kwa timu zinazocheza ugenini dhidi ya klabu kutoka Uarabuni.

Rekodi zinaonyesha kuwa ni vigumu kwa timu kutoka Uarabuni kupoteza mechi ya nyumbani kwenye mashindano ya Afrika kwa ngazi ya klabu pindi inapochezeshwa na N’Diaye mwenye miaka 32.

Aussems ametumia mbinu moja ya kijanja ili kumpunguza makali na kumweka kwenye hofu N’Diaye ili asiwabebe wenyeji katika mchezo huo utakaochezwa Uwanja wa Borg El Arab, jijini Alexandria.

Akizungumza na kituo cha luninga cha cha Sada El-Balad muda mfupi baada ya kutua jijini Alexandria, Aussems amedai anafahamu waamuzi wanaweza kufanya hila za kuhakikisha Ahly inaibuka na ushindi kwenye mchezo huo hivyo, hataumia hata kama Simba ikipoteza.

“Ni mechi muhimu mno. Tunajua tunakutana na timu imara zaidi Afrika kwa kipindi cha miaka 10 ya hivi karibuni. Mechi itakuwa ngumu na tunatakiwa kufanya kazi ya ziada.

“Niwe mkweli. Sikutarajia na sidhani kama tunaweza kupata pointi kutoka kwa AS Vita na Al Ahly kwenye mechi za ugenini. Mkazo wetu ni kukusanya pointi nyumbani.

Huwa sipendelei ndoto. Hatuwezi kupata pointi hapa dhidi ya Al Ahly kwa sababu watapata penalti, mchezaji wetu mmoja ataonyeshwa kadi nyekundu na pia watapewa bao la kuotea,” alisema Aussems.

Kauli ya Aussems inaweza kuchagizwa na matokeo ya mechi ambayo N’Diaye amekuwa akizichezesha timu kutoka Ukanda wa Kaskazini kwenye mataifa yanayozungumza Kiarabu pindi zinapokuwa nyumbani.

Katika msimu wa 2018 na huu wa 2018/2019, N’Diaye amechezesha jumla ya mechi tisa kwenye ardhi ya Uarabuni, ambapo kwenye mechi hizo tisa, timu mwenyeji iliibuka na ushindi mara saba na mechi mbili ziliisha kwa sare.

Miongoni mwa michezo ambayo N’Diaye alilaumiwa kwa kuwabeba wenyeji ni ule wa kwanza wa fainali ya Kombe la Shirikisho baina ya wenyeji Raja Casablanca ya Morocco na AS Vita ya DR Congo. Katika mchezo huo, N’Diaye alimtoa nje kwa kadi nyekundu ya utata beki wa AS Vita, Yannick Bangala na kuizawadia penalti Raja Casablanca ambayo iliwapatia bao lililofanya waibuka na ushindi wa mabao 3-0.

Katika mechi ya marudiano ugenini huko DRC ambayo haikuchezeshwa na refa huyo, Raja Casablanca walichapwa mabao 3-1 lakini hata hivyo, walitwaa ubingwa kwa sheria ya bao la ugenini.

REKODI ZAKE KWA WAARABU 2018/2019.

CS Constantine (Algeria) 1-0 Vipers (Uganda)- Raundi ya kwanza Ligi ya Mabingwa

Wydad Casablanca (Morocco) 5-2 Asec Mimosas (Ivory Coast)- Makundi Ligi ya Mabingwa Afrika.

2018

1. Al-Ahly Shendi (Sudan) 2-1 La Mancha (Congo)- Raundi ya Kwanza Kombe la Shirikisho Afrika.

2. USM Algers (Algeria) 4-0 Plateau United (Nigeria)- Mtoano Kombe la Shirikisho Afrika

3. Raja Casablanca (Morocco) 0-0 AS Vita (DRC)-Makundi Kombe la Shirikisho

4. Al Masry (Misri) 1-0 USM Algers (Algeria)- Robo Fainali Kombe la Shirikisho Afrika

5. Raja Casablanca (Morocco) 3-0 AS Vita (DRC)- Fainali Kombe la Shirikisho Afrika

6. ES Setif (Algeria) 1-1 TP Mazembe (DRC)- Makundi Ligi ya Mabngwa Afrika

7. Etoile Du Sahel (Tunisia) 2-0 Mbabane Swallows (Eswatini)- Makundi Ligi ya Mabingwa

Hali ya hewa

Kikosi cha Simba jana jioni kilianza kujifua ikiwa ni mazoezi yao ya kwanza, lakini kimekumbana na kikwazo cha hali ya hewa ambapo ni baridi kali (nyuzi joto 17) wakati jijini Dar es Salaam ni nyuzi joto kati ya 29-33.

Usalama wa kutosha

Mabosi wa Simba wanajua mbinu zote za kuhakikisha kikosi chao kinakuwa salama wanapokuwa ugenini hasa kwenye ardhi ya Waarabu na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori ameliambia Mwanaspoti kuwa; ,hali ya usalama ni shwari kabisa.

Hata zile figisufigisu ambao wageni wamekuwa wakifanyiwa pindi wanapokanyaga ardhi za Kiarabu kwa ajili ya mechi zao, kwa sasa haipo japo tahadhari zote zimechukuliwa ili kuhakikisha kikosi kiko salama.

Simba imefika hoteli ya Africana jirani kabisa na Uwanja Borg El Arab unaomilikiwa na timu ya Al Ahly, ndiyo watakaoutumia kucheza mechi hiyo ya Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi.

“Tumefikia hoteli ya Africana ambayo ni jirani kabisa na uwanja tutakaochezea mechi hiyo, hali ya usalama mpaka sasa ipo shwari kabisa, hata zile figisufigusi hakuna kwa sasa na kikosi kipo salama tangu tulipowasili,” alisema Magori.



Chanzo: mwananchi.co.tz