Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwameja, Mogella wamtaja mrithi wa Kapombe

28278 Kapombe+pic TanzaniaWeb

Thu, 22 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam.Siku chache baada ya Kocha wa Simba Patrick Aussems kupiga hesabu ya kusajili mchezaji atakayeziba pengo la beki Shomari Kapombe aliyeumia, nyota wa zamani Mohammed Mwameja na Zamoyoni Mogella wamempa mchongo mbelgiji huyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, nyota hao wa zamani wa Simba, walisema kukosekana beki huyo ni pigo, lakini pia ni fursa kwa wachezaji wazawa waliokosa nafasi kuthibitisha ubora wao kwa kuziba pengo la Kapombe.

Kapombe yuko Afrika Kusini kwenye matibabu ya kifundo cha mguu wa kushoto, baada ya kuumia Jumatano iliyopita akiwa katika mazoezi ya timu ya Taifa ‘Taifa Stars’.

Beki huyo wa zamani wa Azam FC aliyewahi kucheza AS Cannes ya Ufaransa, aliumia baada ya kukanyaga mpira vibaya, akiwa na Taifa Stars kambini mjini Bloemfontein, Afrika Kusini.

“Hakukuwa na ulazima wa kocha kwenda kutafuta mbadala wa Kapombe katika usajili wa dirisha dogo, hiyo ilikuwa ni fursa kwa waliokuwa wakikosa nafasi kuthibitisha ubora wao,” alisema Mogella.

Mogella alisema Kapombe ana mchango mkubwa Simba na Taifa Stars, lakini hakuna namna kwa kuwa katika soka majeruhi ni jambo ambalo halikwepeki na ikitokea, lazima apatikane wa kuziba nafasi ya mchezaji aliyeumia.

Mwameja alisema kukosekana Kapombe ni pigo kubwa, lakini Simba ina kikosi kipana. “Ni beki tegemeo, lakini pia hiyo ni fursa kwa wengine kuitumia, wapambane wasisubiri mashabiki waseme pale angekuwepo fulani, wathibitishe ubora wao sasa,” aliongeza Mwameja.

Akizungumza kwa simu jana kutoka Afrika Kusini, Kapombe alisema afya yake inaimarika na anaamini atakuwa vyema na atarejea kazini.

Beki huyo alisema hajui atakuwa nje ya uwanja kwa muda gani kwa kuwa madakatari wanamtibu Afrika Kusini hawajampa taarifa rasmi kuhusu ukomo wake wa kupumzika. Aussems ameanza kupiga hesabu ya kusajili beki wa kuziba pengo la Kapombe.



Chanzo: mwananchi.co.tz