Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwakinyo ataka kuzipiga na bondia Manny Pacquiao

Wed, 27 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Bondia Hassan Mwakinyo amesema anamsubiri bondia nguli duniani, Manny Pacquiao wa Philippines akubali kucheza naye hapo ndipo atawathibitishia Watanzania ubora wake katika mchezo wa ngumi.

Mwakinyo anayeshika namba 19 kwa viwango vya ubora duniani katika uzito wa superwelter, alisema ndoto yake ni kucheza na bondia huyo ambaye jina lake halisi ni Emmanuel Dapidran Pacquiao.

“Siku Pacquiao atakaposema nimekubali kucheza na Mwakinyo najua Watanzania watanielewa nafanya nini,”alisema bondia huyo alipotembelea Ofisi za Makao Makuu ya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Dar es Salaam, jana.

Mwakinyo mwenye rekodi ya kucheza mapambano 17 na kushinda 15, alisema ndoto yake ni kufikia rekodi ya mabondia nyota wa dunia kama Pacquiao mwenye rekodi ya kucheza mapambano 70 na kushinda 61.

“Ninapokwenda ni pakubwa zaidi ya nilipotoka, lakini naamini siku ninayoisubiri kwa hamu ya kucheza na Pacquiao itatimia na ndipo nitawathibitishia Watanzania nini nahitaji katika ngumi,” alisema Mwakinyo anayetoka mkoani Tanga.

Alisema ana ndoto ya muda mrefu katika ngumi na safari yake katika masumbwi inamtuma kuzichapa na mabondia nyota duniani akina Floyd Maywether na Jarret Hurd wenye nyota tano huku yeye akiwa na nyota tatu na nusu.

Mwakinyo alisema kuwa tangu akiwa bondia asiyekuwa na jina, alikuwa na ndoto ya kucheza ngumi za kulipwa licha ya kufanya mazoezi kwa kutumia tairi la gari.

“Niliamini katika ndoto yangu licha ya kufanya mazoezi katika mazingira magumu, lakini niliamini ipo siku nitafanikiwa, mama yangu amekuwa akiniunga mkono sana naomba na wazazi wengine wawaunge mkono watoto wao,” aliongeza Mwakinyo.

Alisema mkakati wake ni kuandaa mashindano ya ngumi za ridhaa ambazo zitawaibua mabondia wenye umri mdogo ambao baadaye watarithi mikoba yake baada ya kustaafu.

Rekodi za mabondia hao zinaonyesha Pacquiao amepigana mapambano 70, ameshinda mara 61 (39 kwa KO), amepigwa mara saba na kutoka sare mara mbili tangu mwaka 1995 alipoingia kwenye ngumi za kulipwa.

Kwa upande wake Mwakinyo amecheza mara 17, ameshinda mapambano 14 (11 kwa KO), amepigwa mara mbili tangu mwaka 2015 alipoingia rasmi katika ngumi za kulipwa.



Chanzo: mwananchi.co.tz