Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwadui yamfungia kazi Kagere Simba

82270 Pic+mwadui Mwadui yamfungia kazi Kagere Simba

Wed, 30 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam/Mwanza. Wakati Patrick Aussems wa Simba akitamba kuendeleza rekodi ya ushindi dhidi ya Mwadui, kocha Khalid Adam amesema ameandaa ulinzi kwa Meddie Kagere.

Simba itakuwa ugenini kuvaana na Mwadui kwenye Uwanja wa CCM Kambarage, Shinyanga ikiwa na rekodi ya kushinda mechi zote sita msimu huu.

Timu hiyo ina pointi 18 na haijafungwa mchezo wowote wa Ligi Kuu Tanzania Bara tangu ilipoanza Agosti 24, mwaka huu.

Akizungumza jana, Aussems alisema timu yake imekuwa ikicheza kwa kiwango bora na leo itaendeleza rekodi hiyo dhidi ya Mwadui.

“Tulicheza vizuri dhidi ya Singida United ingawa uwanja haukuwa mzuri. Tulitengeneza nafasi nyingi lakini tulishindwa kuzitumia, tunatarajia mabao mengi kwa Mwadui,”alisema Aussems.

Wakati Aussems akitoa kauli hiyo, Adam alisema amewapa maelekezo mabeki wake namna ya kumdhibiti Kagere.

Kocha huyo alisema Kagere atalazimika kufanya kazi ya ziada kuwapita mabeki wake watatu tegemeo Joram Mgeveke, Augostino Samson na Khalfan Mbarouk.

“Tunajua ubora wa Kagere lakini haitakuwa kazi nyepesi kwake tayari nimetoa maelekezo kwa mabeki wangu jinsi ya kumdhibiti nina imani watafanya kazi yao vizuri kama watafuata maelekezo yangu,”alisema Adam.

Mwadui inashika nafasi ya 12 katika msimamo imeshinda mechi moja, imetoka sare mara tano na imefungwa michezo miwili.

Simba ndiyo timu pekee haijafungwa na safu yake ushambuliaji ikiweka rekodi ya kufunga mabao 12. Kagere amefunga mabao saba akifuatiwa na Miraji Athumani aliyefunga manne.

Katika mechi nyingine KMC itamenyana na Ruvu Shooting Uwanja wa Mabatini, mchezo ambao kocha Jackson Mayanja alisema utakuwa na ushindani.

KMC imeshinda mchezo mmoja dhidi ya Namungo bao 1-0, lakini kocha huyo alisema anataka kupata pointi tatu.

“Tulikuwa na majeruhi wengi mwanzoni mwa msimu na waliporudi hawakuingia moja kwa moja kwenye programu zangu. Matokeo tuliyopata ni changamoto kwetu,” alisema Mayanja aliyetua KMC kujaza nafasi ya Etienne Ndayiragije.

Mchezo mwingine unaotarajiwa kuwa na msisimo ni ule kati ya Singida United dhidi ya JKT Tanzania utakaochezwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.

Kocha msaidizi wa Singida United, Mathias Wandiba alisema mfumo wa timu hiyo haukuwa mzuri uwanjani, lakini amerekebisha kasoro hizo na wamejipanga kupata ushindi.

“Mfumo wa uchezaji haukuwa mzuri kulikuwa na kasoro, lakini nadhani sasa wachezaji wako katika hali nzuri na wana morali ya kufanya vizuri,”alisema Wandiba.

Chanzo: mwananchi.co.tz