Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mvua yatibua mipango Simba

50439 MORO+PIC

Thu, 4 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mvua iliyonyesha kwa saa kadhaa mkoani Morogoro, imetibua mipango ya Simba baada ya kuahirishwa kwa mchezo wao jana dhidi ya JKT Tanzania katika Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mchezo huo uliopangwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, uliahirishwa na sasa utapangiwa siku nyingine baada ya uwanja huo kujaa maji.

Simba ilikuwa ikipewa nafasi ya kushinda mchezo huo kutokana na rekodi ya kushinda mechi 10 mfululizo za mashindano hayo.

Licha ya waamuzi kusubiri kwa dakika 15 kwa mujibu wa kanuni kuona kama hali hiyo itabadilika, lakini matumaini ya mchezo kufanyika yaligonga mwamba baada ya kujiridhisha haufai kwa mechi.

Akizungumza jana, Katibu wa Chama cha Soka Mkoa wa Morogoro (MRFA), Charles Mwakambaya ambaye pia ni msimamizi wa kituo cha Morogoro alisema wameahirisha mchezo huo kutokana na uwanja kujaa maji.

“Tumeamua tuahirishe mchezo kwa sababu uwanja hautafaa kucheza umejaa maji. Awali tulisubiri kidogo kuona labda maji yangekauka lakini yakaendelea kuwepo uwanjani.

“Kwa kanuni za ligi mechi ilipaswa ichezwe kesho (leo) lakini tumeiangalia na Simba ambayo ina mechi ya kimataifa Jumamosi dhidi ya TP Mazembe na kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), timu inatakiwa icheze mechi moja kwenda nyingine baada ya saa 72, hivyo kama mechi ingeruhusiwa kuchezwa Alhamisi tungekuwa hatujaitendea haki Simba,”alisema Mwakambaya.

Katibu huyo alisema kwa mashabiki waliolipa viingilio kutazama mchezo huo watapewa utaratibu kupitia Shirikisho la Soka Tanzania(TFF). Endapo mchezo ungefanyika na Simba ingeshinda ingefikisha pointi 60, hivyo ingejiweka katika mazingira mazuri ya kutetea ubingwa na kupunguza pengo la pointi dhidi ya Yanga. Simba ina pointi 57 ikiwa pungufu ya pointi 10 dhidi ya Yanga ambayo leo inaikabili Ndanda kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona Mtwara. Hata hivyo, Simba inakuwa na faida kubwa kutokana na kuwa na mechi sita mkononi zaidi ya Yanga iliyocheza mechi 28 na Azam mechi 29. Kama Simba itashinda mechi zote 16 ziliobaki itafikisha pointi 105, Yanga ikishinda 10 itafikisha pointi 97 na Azam ikishinda tisa itafikisha pointi 89.

Katika mechi za jana, Prisons iliichapa Mwadau 2-0, Lipuli ilishinda 2-0 dhidi ya African Lyon, Singida United iliilaza Alliance 2-0, Mbao ilifungwa 1-0 na Biashara United, Coastal ilishinda 1-0 kwa Stand United.



Chanzo: mwananchi.co.tz