Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Muuaji wa Simba asimulia bao lake

82390 Simba+pic Muuaji wa Simba asimulia bao lake

Fri, 1 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam/ Shinyanga. Gerrard Mathias hakuwa akifahamika katika Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini ghafla nyota yake imeng’aa ghafla baada ya jana kuifunga Simba.

Mathias alikuwa nyota wa mchezo baada ya kufunga bao pekee dakika ya 33 akifunga kwa mpira wa kichwa uliomshinda kipa Aishi Manula.

Akizungumza jana, Mathias alisema aliingia uwanjani akiwa na dhamira ya kuifunga Simba ili kuinusuru Mwadui katika msimamo wa ligi.

“Niliingia uwanjani nikiwa na nia ya kufunga, nimefunga bao katika mazingira magumu lakini nilitulia na kuangalia wapi nipeleke mpira,” alisema Mathias ambaye mpura wake ulimshinda Manula na kuangukia wavuni.

Uzembe wa mabeki wa Gerson Fraga na Gadiel Michael ulitoa nafasi kwa Mathias kuruka kuwahi mpira wa krosi uliopigwa kutoka upande wa kushoto.

Mwadui ikiwa Uwanja wa Kambarage, ilicheza kwa kiwango bora dakika zote 90 za mchezo huo na kushinda bao 1-0 na Omari Abdallah, Ludovick Evance na Mathias walitoa presha kubwa kwa safu ya ulinzi ya Simba na mara kwa mara ilipwaya. Mathias amefikisha mabao manne baada ya lile la awali alilowafunga Coastal Union msimu huu.

Mipango ya viungo Mzamiru Yassin, Clatous Chama ilitibuliwa na Mussa Nampaka na Emmanuel Memba ambao walitibua mipango yao, huku beki wa kati Joram Mgeveke wa Mwadui alicheza lwa nidhamu eneo la ulinzi akicheza sambamba na Augostino Samson, alimdhibiti vizuri Meddie Kagere ambaye alikuwa akihaha akitaka kufunga.

Mwadui aliwatumia mabeki wa pembeni Khalfan Mbaruku na Rogers Gabriel kupeleka mashambulizi langoni mwa Simba kwa kupiga krosi nyingi.

Mabeki wa pembeni wa Simba Haruna Shamte na Gadiel hawakuwa katika ubora wao kwani mara kwa mara waliruhusu mipira ya krosi ya kina Hassan Kapalata.

Simba ilikuwa timu pekee ambayo ilikuwa haijafungwa katika mechi sita ilizocheza ikifunga mabao 12. Kagere amefunga saba akifuatiwa na Miraji Athumani aliyefunga manne.

Wakati Simba bado inaongoza katika msimamo wa Ligi Kuu kwa pointi 18, Mwadui inayonolewa na Kocha Khalid Adam imefikisha 11.

Rekodi inaonyesha mechi za Kanda ya Ziwa, Simba ilishinda mabao 2-0 dhidi ya Biashara United mjini Musoma kabla ya kuilaza Kagera Sugar 3-0 na Kagera Sugar Uwanja wa Kaitaba.

Msimu uliopita Simba ilifungwa na Kagera Sugar mabao 2-1, ilichapwa na Mbao bao 1-0 kabla ya kuilaza Biashara 2-0. Iliifunga Alliance 2-0, iliilaza Stand United 2-0 kabla ya kuichapa Mwadui 3-1. Msimu wa 2016/2017 Simba ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Stand United na iliichapa bao 1-0 na Kagera Sugar.

Mwadui: Mahmoud Amir, Rogers Gabriel, Khalfan Mbaruku, Agustino Samson, Joram Mgeveke, Emanuel Memba, Hassan Kapalata, Musa Nampaka, Omar Abdallah, Gerald Mathias na Ludovick Evance.

Simba: Aishi Manula, Haruna Shamte, Gadiel Michael, Erasto Nyoni, Tairone Santos, Gerson Fraga, Clatous Chama, Mzamiru Yassin, Meddie Kagere, Sharaf Shiboub na Francis Kahata.

Matokeo mengine, Kagera Sugar ilishinda mabao 2-0 dhidi ya Namungo na kufikisha pointi 16 ikiwa nafasi ya pili nyuma ya Simba. Ruvu Shooting iliilaza 1-0 KMC Mtibwa ilishinda 2-1 dhidi ya Coastal Union.

Lipuli iliifunga Polisi Tanzania mabao 2-1, Singida United iliendelea kugawa pointi baada ya kuchapwa 2-1 dhidi ya JKT Tanzania.

Chanzo: mwananchi.co.tz