Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mukoko arudi na mkwara, Nabi aipangia KMC ukuta mpya

Mukooo Pic Data Mukoko arudi na mkwara, Nabi aipangia KMC ukuta mpya

Sat, 9 Oct 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

HABARI njema kwa mashabiki wa Yanga ni kurejea kwa kiungo wao, Mukoko Tonombe ‘Teacher’, baada ya kumaliza adhabu yake ya kukosa mechi tatu na ametamka wazi sasa anaitaka namba yake katika kikosi cha kwanza.

Kiufundi wadau wanasema ujio wa staa huyo unamtega Kocha Nasreddine Nabi ambaye huenda akalazimika kupangua safu ya ulinzi kwa kuanzia na mechi na KMC.

Mukoko alikosa mechi tatu zilizopita mbili za Ligi Kuu Bara na mchezo mmoja wa Ngao ya jamii kutokana na adhabu ya kadi nyekundu aliyopewa kwenye Fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Simba msimu uliopita uliopigwa mkoani Kigoma na chama lake kulala kwa bao 1-0.

Kiungo huyo, sasa yupo huru kuanza kuitumikia Yanga kuanzia mchezo ujao dhidi ya KMC utakaopigwa Uwanja wa Majimaji Songea na hatua hiyo itarudisha vita mpya ya namba katika safu ya ulinzi na ile ya kiungo anayocheza, akimtega Kocha Nabi ambaye sasa atalazimika kupangua kikosi chake kwa mechi zijazo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mukoko alisema bado ana nafasi ya kucheza katika timu hiyo ingawa amekiri kwa sasa kuna ushindani mkubwa wa nafasi ndani ya timu hiyo tangu kutua kwa Khalid Aucho kutoka Uganda na beki kiraka Yannick Bangala aliyesajiliwa kutoka DR Congo.

“Nimekuwa nikifanya mazoezi makali nijiweke sawa, kwa sasa niko sawa kuanza kazi msimu huu, najua kuna ushindani mkubwa, ila najiamini uwezo wangu ndio utaamua nafasi yangu makocha wataamua,” alisema Mukoko ambaye ni Nahodha Msaidizi wa timu hiyo.

Tangu msimu huu uanze kocha Nabi amekuwa akiwatumia Aucho na Bangala katika safu ya kiungo lakini sasa huenda mambo yakabadilika.

Hata hivyo kurejea kwa Mukoko kunaweza kukashusha presha baada ya Nahodha Mkuu wa timu hiyo, beki Bakari Mwamnyeto kupata maumivu na kama ataendelea kuwa nje.

Baada ya Mwamnyeto kukosa mechi mbili za ligi Nabi amemrudisha Bangala katika nafasi yake ya beki wa kati akicheza sambamba na Dickson Job na katika mechi tatu zilizopita alizokosa Mukoko kucheza Bangala, Mwamnyeto na Aucho wameilinda ngome hiyop bila kuruhusu bao lolote.

WASIKIE WADAU

Kiungo wa zamani wa Yanga, Athuman Idd ‘Chuji’ alisema kurejea kwa Mukoko kutaleta vita mpya. Chuji alisema vita hiyo haitaweza kumweka nje Bangala wala Aucho lakini akahofia kati ya mabeki Mwamnyeto na Job huenda mmoja akapoteza nafasi.

“Unajua Yanga msimu huu wanatimu bora sana na hii ya kurejea kwa Mukoko kutaleta vita mpya pale Mukoko ameona jinsi safu ya Yanga ilivyotulia kwahiyo ana kazi kubwa ya kuwa bora ili alinde nafasi yake,” alisema Chuji ambaye alikuwa anacheza nafasi za kiungo na hata beki.

“Sioni kama itakuwa rahisi kwa kocha kumweka nje Bangala ameonyesha ni beki mzuri, lakini pia anaweza kucheza kiungo wasiwasi wangu ni ubora kati ya Mwamnyeto na Job wanatakiwa kuwa bora sio tu kuzuia pia kuanzisha mashambulizi,” alisema Chuji na kuongeza;

“Siku hizi beki sio kazi yake kuzuia tu anatakiwa pia kupandisha mashambulizi sasa hapo atakayekuwa bora kati ya wote Mwamnyeto, Job, Mukoko na Aucho ndio atapata nafasi,” alisema Chuji aliyewahi kukipiga Polisi Dodoma, Simba, Coastal Union, Singida United na Taifa Stars kwa vipindi tofauti na kuwa gumzo kwa mashabiki wa soka nchini.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz