Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Muda wa wakali wa kubet sasa ndio huu umewadia

11735 Goshashi+allan TanzaniaWeb

Mon, 13 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Michezo ya kubahatisha ni moja ya shughuli za kiuchumi zinazoendeshwa kwa mujibu wa sheria kama zilivyo shughuli nyingine. Pia, ni miongoni mwa biashara ambazo zinachangia pato la Taifa.

Kwa mujibu wa sheria, hakuna mtu au taasisi inayoruhusiwa kuendesha biashara ya Michezo ya Kubahatisha bila kuwa na leseni kutoka Bodi ya Michezo ya Kubahatisha pamoja na vibali vingine vinavyotolewa na mamlaka zingine za biashara.

Pia, sheria inakataza watoto wenye umri chini wa miaka 18 kushiriki, kuingia, kukaa au kuzururazurura karibu na maeneo ya michezo ya kubahatisha.

Ninafahamu pia dini mbalimbali hazikubali michezo ya kubahatisha na zina sababu zake, lakini ukweli unaposhiriki mara kwa mara kwenye michezo hii ina asili ya matumizi mabaya ya fedha. Ijapokuwa kuna mambo mengi ambayo yanaweza kuleta matumizi mabaya ya fedha.

Hata hivyo, ninavyofahamu ni kwamba michezo ya kubahatisha inaweza kubadilisha maisha ya mtu wakati wowote kama mtu anaweza kubashiri vizuri.

Kwa mfano hivi sasa mchezo wa kubahatisha katika mechi mbalimbali za soka za ligi tofauti umeshika kasi kutokana na ongezeko la vituo vya kamari ya soka maarufu kama ‘kubeti’.

Watu wa umri tofauti nchini wanashiriki katika mchezo huu na wale wanaobahatika kubashiri vizuri matokeo ya timu ndivyo wanavyopata fedha huku wengine wakiliwa fedha nyingi.

Ieleweke kwamba watu wengi wameingia katika mchezo huu kwa sababu ya kutaka fedha za haraka kwa ajili ya kuendesha maisha.

Ndiyo, wote tunafahamu kwamba hali ya maisha ni ngumu kwa hiyo watu wanatafuta njia mbalimbali mbadala za kujiongezea kipato ikiwamo kushiriki katika michezo ya kubahatisha ‘kubeti’.

Michezo hii, imekuwa ni chanzo cha kipato kwa vijana wengi hasa wa Dar es Salaam ambapo kampuni nyingi za michezo hii zinafanya shughuli zake.

Hii inatokana na kiwango cha fedha kinachotumika katika michezo hiyo ni kidogo ukilinganisha na kiwango ambacho mtu anakipata baada ya kupatia matokeo ya michezo aliyobashiriri.

Kiwango cha chini cha kucheza mchezo huu kwenye kampuni nyingi za kubeti hapa nchini ni Tsh 500, ambacho vijana wengi wanaweza kukimudu na kupitia kiwango hicho mtu anaweza kushinda mpaka Tsh laki moja (100,000) kama tu atapatia matokeo kwa usahihi.

Ifahamike kwamba hapa nchini mchezo huu wa kubahatisha hufanyika kwa ligi za kimataifa huku Ligi Kuu ya England (EPL), Ligi Kuu ya Hispania (La Liga), Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga), Ligi Kuu ya Italia (Serie A) na Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) zikiwa maarufu zaidi na zinazovutia watu wengi pamoja na michezo ya timu za Taifa.

Hata hivyo, ligi hizi zilikuwa zimesimama kwa sababu ya kumalizika kwa msimu wa 2017-2018, hivyo watu wengi walizitumia Fainali za Kombe la Dunia 2018 kubeti na zenyewe zimeisha tangu mwezi wa saba.

Hivi sasa, mashabiki wa soka nchini na wale wanaoshiriki mchezo wa kubeti wameanza kufurahia tena kwani Ligi Kuu mbalimbali wanazozishabikia na zinazowapa fedha nyingi mojawapo ikiwa Ligi Kuu England zimeanza jana.

Ligi Kuu ya England (EPL) imeanza Agosti 10, 2018, Ligi Kuu ya Hispania (La Liga) inaanza Agosti 17, 2018, Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) inaanza Agosti 24, 2018.

Pia kuna Ligi Kuu ya Italia (Serie A) inaanza Agosti 19, 2018 na Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) ambayo imeanza jana Agosti 10, 2018. Zote watu wanasubiri kupiga pesa.

Chanzo: mwananchi.co.tz