Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtibwa yabeba ubingwa U20

F1f3a64053597beeb33948861004f388 Mtibwa yabeba ubingwa U20

Mon, 21 Jun 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

TIMU ya soka ya vijana ya umri chini ya miaka 20 ya Mtibwa Sugar imetetea ubingwa wake wa Ligi Kuu ya vijana baada ya kuifunga Yanga kwa mabao 2-1, katika mchezo wa fainali uliochezwa Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Dar es Salaam.

Hilo ni taji la tatu mfululizo kwa Mtibwa Sugar ambao walionesha ubora mkubwa ikilinganishwa na timu nyingine zilizoshiriki michuano hiyo msimu huu.

Kwa upande wa tuzo, kiungo bora wa michuano hiyo na mchezaji bora wa mashindano ilikwenda kwa Joseph Mkele wa Mtibwa Sugar na mshambuliaji bora, Omary Malungu wa Mtibwa akiwa amefunga mabao sita.

Kipa bora ni Godfrey Magaigwa wa Yanga na beki bora wa mashindano ilikwenda kwa Ally Said wa Yanga, wakati Awadhi Juma kutoka Mtibwa Sugar alibeba tuzo ya kocha bora na tuzo ya timu yenye nidhamu ilikwenda kwa wenyeji Azam FC iliyomaliza nafasi ya nne kwenye michuano hiyo.

Tuzo ya mwamuzi bora wa michuano hiyo ilichukuliwa na Hussein Katanga, wakati Triphina Tryphone alitwaa tuzo ya mwamuzi bora msaidizi.

Akizungumza baada ya mchezo wa fainali kumalizika, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF), Wallace Karia alisema michuano hiyo imekuwa na faida kwa klabu kuona uwezo walionao vijana na kuwapa nafasi ya kuwapandisha kwenye timu zao kubwa ili kupunguza gharama za kusajili wachezaji wa kigeni.

“Nimeshuhudia vipaji vingi kupitia michuano hii, siyo vibaya kama makocha watawapa nafasi kwenye timu za wakubwa msimu ujao lakini hata kwa timu zetu za taifa tuna hazina kubwa ya vijana ni lazima klabu zihakikishe zinawajenga utaratibu maalumu wa kutunza vipaji hivyo kwa maslahi ya taifa,” alisema Karia.

Kwa upande wake, kocha wa Mtibwa, Awadhi Juma alisema anajiona mwenye bahati kwa kupewa jukumu hilo na uongozi wa klabu yake na kutetea taji hilo.

Alisema mashindano yali kuwa magumu lakini mchezo wa fainali ndio ulikuwa mgumu zaidi hasa kipindi cha pili ambacho Yanga walikuja juu na kutaka kusawazisha.

“Ni michuano mizuri, niwapongeze wachezaji wangu kwa kufuata maelekezo niliyowapa hadi kutwaa taji hili pia nawapongeza viongozi wangu wa Mtibwa kwa imani yao kwangu, kazi haikuwa rahisi lakini nashukuru kwa kulirudisha taji nyumbani,” alisema Awadhi.

Naye Kocha wa Yanga, Said Maulid ‘SMG’ aliwapongeza wachezaji wake kwa kupambana na kufika fainali, lakini alimtupia lawama mwamuzi wa mchezo huo kwa kukataa bao lao la kusawazisha na kusema mchezaji Abdulikarim Yunusi hakuwa ameotea.

“Nawapongeza wachezaji wangu wamefanya kazi kubwa kuanzia mechi za awali hadi fainali, niseme hatukuwa na bahati kwa sababu licha ya kutanguliwa lakini vijana walitulia na kucheza vizuri na kufanikiwa kurudisha mabao ingawa bao letu la kusawazisha mwamuzi alilikataa, niwashukuru TFF na uongozi wa Yanga kwa msaada waliotupa,” alisema SMG.

Chanzo: www.habarileo.co.tz