Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtibwa wampotezea Makambo

13430 MAKAMBO+PIC TanzaniaWeb

Thu, 23 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati Yanga leo itashuka dimbani kuanza kampeni za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2018/19 kwa kuikaribisha Mtibwa Sugar ya Morogoro kwenye Uwanja wa Uhuru, hatma yake ipo miguuni mshambuliaji mpya, Heritier Makambo kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Makambo aliyesajiliwa na Yanga akitokea FC Lupopo ya DR Congo, amebeba matumaini makubwa ya wanachama na mashabiki wa Yanga kutokana na uwezo mkubwa aliouonyesha tangu ajiunge na timu hiyo.

Mchezaji huyo amekuwa mahiri kuzifumania nyavu tangu mazoezini hadi katika mechi za kujipima nguvu na alithibitisha makali yake katika mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya USM Algiers ya Algeria alipofunga bao murua kuiwezesha Yanga kushinda kwa mabao 2-1.

Mshambuliaji huyo aliipasua ngome ya USM Algiers wakati mgumu kiasi kwamba beki yao ilishindwa kuendeleza utaratibu wao wa kupandisha mashambulizi kwa kumuhofia.

Uhodari na uwezo wake wa kuzifumania nyavu umeipa matumaini Yanga na sasa hawawafikirii tena akina Donald Ngoma aliyeenda Azam wala Obrey Chirwa aliyetimkia Misri.

Katika mechi sita ambazo Makambo ameichezea Yanga dhidi ya timu za Transit Camp, Tanzanite Academy, Mawenzi Market na Mkamba Rangers ambazo zilikuwa za kirafiki na ile dhidi ya USM Algiers kwenye hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, ameifungia Yanga mabao matatu.

Mshambuliaji huyo amekuwa gumzo nchini kwa sasa kutokana na kiwango alichokionyesha hasa katika mchezo dhidi ya USM Algiers.

Ubora wake katika kutengeneza nafasi, kumiliki mpira na kuwatoka mabeki, unaweza kuwa chachu ya ushindi atakapoungana na mawinga viberenge, Mrisho Ngassa, Deusi Kaseke, Emmanuel Martin au Juma mhadhi, ambapo yeye atasaidiwa na Hamisi Tambwe, Matteo Anthony au Ibrahim Ajibu katika safu ya ushambuliaji.

“Usajili wa Makambo ni usajili mzuri na naamini yeye pamoja na wenzake wapya watakuwa na mchango mkubwa kwenye timu wakiunganisha nguvu na wale waliokuwemo kikosini tangu awali. Sio jambo jema kumzungumzia mchezaji mmoja mmoja lakini kiufupi naamini Makambo atatusaidia sana,” alisema Kocha Msaidizi wa Yanga, Noel Mwandila.

Kwa upande wa Mtibwa Sugar, ambao wamekuwa wakiipa Yanga wakati mgumu zinapokutana katika mechi za Ligi Kuu, tayari imetamba kuwa hawana hofu na mshambuliaji huyo na wamejipanga kumdhibiti leo.

“Hivi kwa nini tumuhofie mchezaji mmoja, sisi tunapocheza na Yanga na tunahitaji ushindi na hatumuohofii yoyote, tunajua tukishinda mechi ya kwanza ya ligi msimu huu itatufungulia njia ya kushinda michezo mingie ijayo,” alisema Kocha wa Mtibwa, Zuberi Katwila.

“Najua Yanga ni timu kubwa na nzuri na ilionyesha kiwango kikubwa dhidi ya USM Algiers, Makambo alicheza vizuri lakini hatutishi,” alitamba Katwila.

Pamoja na tambo za Katwila, safu ya ulinzi ya Mtibwa itakuwa kwenye wakati mgumu muda mwingi wa mchezo huo.

Namna Yanga itakavyocheza katika safu ya kiungo na ushambuliaji, ndivyo inavyoweza kuibuka na ushindi.

Kikosi hicho kinajivunia sana uimara wa safu ya ulinzi inayoundwa na kipa Beno Kakolanya, Juma Abdul, Gadiel Michael, Kelvin Yondan (Nahodha) na Andrew Vincent ‘Dante’.

Kama itacheza kama ilivyokuwa na USM Algiers katika kiungo Yanga itakuwa na Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Papi Kabamba Tshishimbi na Raphael Daud au Pius Buswita, inaweza kupata matokeo.

Yanga itaingia kwenye mchezo huo ikitaka kulipa kisasi baada ya kupoteza pointi tano dhidi ya Mtibwa msimu uliopita, kwani zitoka sare ya bila kufungana kwenye mchezo wa kwanza kabla ya kufungwa bao 1-0 ugenini kwenye mzunguko wa pili.

Safu ya kiungo ya Mtibwa inaendelea kuongozwa na mkongwe Shaaban Nditi kwa karibu msimu wa saba sasa na mar azote anawatesa viungo wa Yanga.

Kocha Msaidizi wa Yanga, Noel Mwandila aliliambia gazeti hili kuwa licha ya kuipa heshima Mtibwa, Yanga imejipanga kuvuna pointi tatu.

Mbali ya mechi hiyo ya Yanga na Mtibwa, mechi nyingine zitakazochezwa leo ni kati ya JKT Tanzania itakayoikaribisha KMC ya Kinondoni, Azam FC itaialika Mbeya City kwenye Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam, wakati Stand United itaikaribisha African Lyon ya Dar es Salaam, kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

Mechi za ufunguzi jana, Coastal Union na Lipuli zilitoka sare ya 1-1. Jijini Mwanza, wageni wa ligi hiyo, Alliance walionja chungu baada ya kupigwa bao 1-0 na Mbao FC sawa na Ruvu Shooting waliofungwa idadi hiyo na Ndanda.

Mjini Bukoba, Kagera iliilaza Mwadui FC mabao 2-1. Biashara Mara ilianza kwa kuilaza Singida 1-0 mjini Musoma.

Chanzo: mwananchi.co.tz