Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtibwa, Yanga ngumu kumeza

5d379491f9145d99497030f48f5d06c1 Mtibwa, Yanga ngumu kumeza

Wed, 22 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MCHEZO wa Yanga dhidi ya Mtibwa Sugar ni kati ya mechi nne za Ligi Kuu Tanzania Bara za leo ambazo ni ngumu na timu hizo zinahitaji matokeo mazuri kujua hatma ya nafasi walizopo.

Yanga itakuwa ugenini kuwakabili wenyeji Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro, mchezo ambao unatolewa macho kutokana na umuhimu wa kila mmoja kupigania matokeo mazuri.

Mabingwa hao wa kihistoria wanataka pointi tatu kuendelea kubaki katika nafasi ya pili na wenyeji wanataka matokeo hayo kujiweka katika nafasi salama na kujiondoa kwenye kushuka daraja.

Yanga yenye pointi 68 ikifungwa au kupata sare itakuwa kwenye presha kwa sababu nyuma yake kuna Azam FC yenye pointi 66 ambao watacheza kesho na wakishinda wanaweza kuishusha.

Mtibwa iko katika nafasi ya 14 kwa pointi 41 na itakuwa hatarini zaidi iwapo watashindwa kupata matokeo mazuri na walioko chini yake wakishinda wanaweza kumshusha chini.

Timu zote mbili zinakutana zikitoka kupata matokeo yasiyoridhisha katika michezo yao iliyopita, Yanga ikilazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Mwadui na Mtibwa ikifungwa na KMC nyumbani bao 1-0.

Mara nyingi timu hizo zinapokutana bila kujali kiwango cha kila mmoja, ushindani unaongezeka. Yanga ilishafungwa mara mbili kwenye Uwanja wa Jamhuri mwaka 2018 na 2019 na wao kushinda mara moja mwaka 2015 na kupata suluhu moja mwaka 2017.

Mchezo mwingine mgumu ni Mbao dhidi ya Namungo utakaochezwa CCM, Kirumba, Mwanza.

Wenyeji wanashika nafasi ya pili kutoka mwisho wakiwa na pointi 39, wanahitaji kushinda kuendelea kufufua matumaini kama watabaki kulingana na matokeo mengine yatakavyokuwa.

Mbao katika michezo mitano iliyopita haijapoteza mchezo hata mmoja, imeshinda minne na kupata sare moja. Na Namungo inayoshika nafasi ya nne, iko kwenye mbio za kuwania nafasi ya pili, kwa pointi 64 na wote wanahitaji matokeo.

Nyingine ni Mwadui dhidi ya Biashara utakaochezwa Mwadui Complex, Shinyanga. Mwenye presha ni mwenyeji aliyeko nafasi ya 16 kwa pointi 41 anahitaji ushindi kutoka hatarini la sivyo, akiruhusu kufungwa mambo yatazidi kuwa mabaya.

Kuna KMC itakayochuana na Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Uhuru Dar es Salaam. Wote wawili wanahitaji matokeo kujihakikishia nafasi ya kubaki salama.

KMC inashika nafasi ya 11 kwa pointi 46 na Prisons nafasi ya 12 kwa pointi 45. Wakishinda au kutoka sare wanaweza kubakia walipo au kushuka kidogo kutegemea na walioko chini yake watatokaje katika mechi zao.

Mbali na hao, mchezo mwingine utakaochezwa ni Singida dhidi ya Kagera ambao wenyeji washinde au wafungwe hawaendi popote kwani tayari wameshashuka daraja labda kwa mgeni matokeo ni muhimu kujiimarisha katika nafasi za katikati.

Chanzo: habarileo.co.tz