Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtibwa Sugar, Mbeya City watambiana

Cbcb94b0c2d95b2c2965ab83a01317ac.jpeg Mtibwa Sugar, Mbeya City watambiana

Mon, 17 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

BAADA ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons, kaimu kocha mkuu wa Mtibwa Sugar, Vicent Barnabas ametamba kuendeleza wimbi la ushindi nyumbani watakapowaalika Mbeya City kesho katika Uwanja wa Jamhuri Morogoro.

Kocha huyo alisema kuwa ushindi wa bao 1-0 walioupata umewasogeza hadi nafasi ya 14 katika msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara wakiwa wamejikusanyia pointi 31 baada ya kushuka uwanjani mara 29.

Akizungumza na gazeti hili, Barnabas alisema kuwa wanaiheshimu Mbeya City ni timu nzuri ambayo hivi sasa inafanya vizuri ndio maana ipo juu yao, lakini hilo halitawazuia kuondoka na pointi tatu katika mchezo ujao ili kupanda juu ya msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.

“Ushindi dhidi ya Tanzania Prisons, umeongeza kitu katika kikosi chetu tunaendelea kupambana ili kujiweka katika nafasi nzuri zaidi kwenye msimamo wa Ligi,” alisema Barnabas.

Naye Kocha Mkuu wa Mbeya City, Mathias Lule amesema kuwa malengo yao ni kuondoka na pointi tatu katika kila mchezo watakaoshuka uwanjani haijalishi wako nyumbani au ugenini, hivyo Mtibwa Sugar wajiandae kuachia pointi tatu.

“Tumekuwa na muendelezo mzuri wa matokeo naamini tutaendelea hivi katika michezo yote iliyosalia, kwani tayari timu yangu imepata muunganiko mzuri ,” alisema Lule.

Mbeya City hivi sasa ipo katika nafasi ya 11 katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikiwa na pointi 33 baada ya kushuka uwanjani mara 29 na kuondoka katika eneo la kushuka daraja.

Chanzo: www.habarileo.co.tz