Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtendaji mkuu mpya Simba SC aanza na Kiswahili

74743 Simba+pic

Mon, 9 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Simba SC imeanza mabadiliko ya kuunda sekretarieti mpya baada ya jana kumtambulisha mtendaji mkuu mpya, Senzo Mazingiza ambaye ameahidi kuiwezesha klabu hiyo kuwa na mafanikio kibiashara na hata ndani ya uwanja.

Mazingiza, raia wa Afrika Kusini aliyeanza kujifunza lugha ya Kiswahili, anachukua nafasi hiyo iliyokuwa ikishikiliwa na Crescentius Magori ambaye amekaa pembeni baada ya kuombwa na bodi ya klabu hiyo.

Akizungumza katika Hoteli ya Serena wakati wa utambulisho, Magori alisema Mazingiza amepata nafasi hiyo baada ya kushinda katika mchakato uliowashindanisha watu wanane walioomba, huku sita wakiwa wazawa na wawili wageni kutoka Afrika Kusini na Amerika.

Magori alisema baada ya mchakato aliousimamia mwenyewe, kamati maalumu ya mchujo iliwapitisha watu wawili na hatimaye Mazingiza akashinda nafasi hiyo.

Alisema Mazingiza ni mgeni katika kufanya kazi nchini, lakini si mtu mpya kwani amewahi kufanya kazi kama hiyo katika klabu za Afrika Kusini ikiwemo Orlando Pirates na Platinum FC, na pia alikuwa mmoja wa maofisa waliokuwa kwenye kamati ya usimamizi wa Kombe la Dunia lililofanyika nchini humo 2010.

Akizungumza baada ya utambulisho huo, Mazingiza ambaye alianza kwa kuzungumza maneno machache ya Kiswahili akisema ni lugha iliyopitishwa na Nchi za Jumuiya ya Kiuchumi Kusini mwa Afrika (Sadc) kutumika katika ukanda huo, alisema ni heshima kubwa kwake kufanya kazi katika klabu kubwa barani Afrika.

Alisema katika majukumu yake atajituma ili kufanikisha klabu hiyo kuwa na mafanikio kibiashara na uwanjani akishirikiana na kila mmoja wakiwemo mabosi wake, wanachama, mashabiki na timu kwa ujumla.

Chanzo: mwananchi.co.tz