Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtanzania atwaa medali, afuzu mbio za dunia

19067 Pic+medali TanzaniaWeb

Mon, 24 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mwanariadha wa Tanzania, Failuna Abdi ametwaa medali ya fedha katika mashindano ya mbio za marathoni zilizofanyika Afrika Kusini.

Matokeo hayo yamempa Failuna tiketi ya kushiriki mbio zijazo za dunia zinazotarajiwa kufanyika nchini Qatar.

Failuna jana aliitoa Tanzania kimasomaso kwenye mbio za Sanlam Cape Town Marathoni alipotumia saa 2:29:59 kumaliza, akiachwa kwa sekunde 32 tu na bingwa wa medali ya dhahabu raia wa Namibia, Helalia Johannes aliyetumia saa 2:29:27.

Katika mbio hizo, Failuna aliwabwaga wanariadha wa Ethiopia na Kenya nchi zinazosifika kufanya vizuri kwenye mbio ndefu duniani.

“Yalikuwa ni mashindano magumu lakini maandalizi na kujiamini ndivyo vimenipa ushindi,” alisema Failuna muda mfupi baada ya kuibuka mshindi wa pili.

Akizungumza kwa simu jana, mwanariadha huyo alisema alijipanga kushinda dhahabu, lakini alizidiwa mbinu na Mnamibia aliyemzidi kasi sekunde chache kabla ya kumaliza mbio hizo.

Nafasi ya tatu ilichukuliwa na Muethiopia, Urge Diro aliyekimbia kwa saa 2:30:30.

Ushindi huo umempa tiketi Failuna kushiriki mashindano ya dunia yatakayofanyika Septemba, mwakani kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Khalifa mjini Doha.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Wilhelim Gidabuday alisema ushindi wa Failuna ni matokeo mazuri na muendelezo wa wanariadha Tanzania kufanya vyema miaka ya hivi karibuni.

Gidabuday alisema matokeo aliyopata Failuna yanadhihirisha Tanzania imeanza kurejea kwenye rekodi ya kimataifa.

Kocha wa riadha Arusha, Thomas Tlanka alisema muda aliokimbia Failuna ni mzuri na umetoa taswira njema kwa Tanzania kwenye mashindano hayo yanayotambuliwa na Shirikisho la Riadha la Kimataifa (IAAF).

“Ushindi wa Failuna ni faraja kwa Tanzania, hii ni ishara njema kwa Tanzania,” alisema Tlanka.

Failuna ni miongoni mwa wanariadha wa kike nchini wanaofanya vizuri kwenye mashindano ya ndani ya nchini.

Chanzo: mwananchi.co.tz