Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msuva aeleza Ruge alivyomuibua THT

44418 Pic+msuva Msuva aeleza Ruge alivyomuibua THT

Sun, 3 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Saimon Msuva amesema kifo cha Ruge Mutahaba kimemkumbisha wosia aliopewa wakati akiwa mnenguaji wa Kundi la THT.

Msuva anayeichezea Difaa El Jadida ya Morocco, alisema Ruge ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group ndiye aliyemuibua katika safari yake ya soka.

Msuva alisema anakumbuka Ruge katika mazungumzo yao akiwa Kundi la THT alimtaka kufanya kazi kwa bidii na kutokata tamaa kwa kuwa ana kipaji cha muziki na soka.

“Nakumbuka Ruge alikuwa akiniambia kukata tamaa ni dhambi inayotafuna taratibu. Ni ngumu kumrudisha nyuma mtu asiyekata tamaa, anaweza kuanguka mara nyingi lakini ipo siku atashinda,” alisema Msuva kwa simu jana.

Nyota huyo wa zamani wa Yanga alisema kauli ya Ruge ilimpa hamasa ya kugeukia soka, lakini nako alikutana na changamoto kubwa ya kupata namba katika kikosi cha kwanza.

“Nilivyokuwa Yanga kuna kipindi nilikuwa nazomewa nashukuru Mungu nilikuwa mvumilivu hatimaye nikawa mmoja wa wachezaji muhimu kwenye timu na mashabiki waliokuwa wakinizomea wakaanza kunishangilia,”alisema Msuva.

Mwili wa Ruge unatarajiwa kuwasili nchini leo ukitokea Afrika Kusini ambako kesho utaagwa kabla ya kusafirishwa kwenda Bukoba kwa maziko Jumatatu.



Chanzo: mwananchi.co.tz