Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msolla atamba kutimiza aliyoahidi Yanga  

C03176c95aeb7d6146f3eb05c4b9f3f5.jpeg Msolla atamba kutimiza aliyoahidi Yanga  

Wed, 14 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

IKIWA imetimia miaka miwili tangu alipochaguliwa kuwa mwenyekiti wa Yanga, Dk Mshindo Msolla amesema tayari ametimiza ahadi alizozitoa kwa asilimia 80 kilichobaki ni kumalizia sehemu iliyobaki.

Msolla ambaye alichaguliwa kuiongoza Mei 6, 2019 akipokea kijiti kutoka katika uongozi wa mpito baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo Yusuph Manji kujiuzulu wadhifa huo Mei 27, 2017.

Akizungumza katika kituo cha Channel Ten juzi, Msolla alisema wakati anaomba ridhaa ya kuiongoza Yanga, alitoa ahadi tano ambazo ni kuleta umoja ndani ya timu na kuisogeza zaidi kwa wananchi, kubadiri mfumo wa uendeshaji, kuendeleza miradi aliyoikuta na kuanzisha mingine, Utawala bora pamoja na kujenga timu yenye ushindani.

"Tuliipeleka timu karibu na wananchi kwa kuwataka wanachama wa mkoa husika kuigharamia timu pindi inapokuwa mkoani hapo, lakini pia tangu mwaka 2010 Yanga ilikuwa ikihitaji kuingia katika mfumo wa mabadiliko ya uendeshaji ilikuwa inashindikana lakini hivi sasa mambo yanaenda vizuri tukishirikiana na GSM...

"Mchakato wa mabadiliko unaendelea vizuri tukishirikiana na timu ya Sevilla pamoja na Laliga tukishirikiana kwa ukaribu na GSM...

"Wakati naingia madarakani nilikuta timu inaendelea na mradi wa kujaza kifusi katika Uwanja wa Kaunda hadi sasa zoezi hilo linaendelea liko mbioni kukamilika, lakini pia tunaendelea na ukarabati wa Jengo, tumeanzisha duka la klabu, tuna mpango wa kuanzisha gazeti la timu litakalokuwa linatoka kila wiki…

"Tumekuwa na Utawala bora hasa mchakato wa ajira na manunuzi tumekuwa tukitangaza wazi na kutoa huduma nzuri lakini pia timu zetu zimeongezeka upinzani kuanzia timu za vijana kuanzia chini ya umri wa miaka 17 na 20, timu ya wanawake pamoja na timu kubwa ya wanaume," alisema Msolla.

Alisema anawashukuru GSM na Taifa Gas kwa kuwasaidia katika kipindi chote alichokuwa madarakani kwani wakati anaingia madarakani Yanga, ilikuwa katika hali mbaya lakini kupitia wao mambo yamekua vizuri.

Alisema mihemko ya mitandao ya kijamii ilimtia katika wakati mgumu ambapo ilimtuhumu kuwa ana mapenzi na Simba sababu alivaa jezi nyekundu katika picha ya miaka 25 iliyopita na kuibua taharuki kwa wapenzi wa Yanga.

"Walidhani jambo hili lingetuvuruga lakini Yanga hivi sasa ina umoja wa asilimia 95 kuanzia viongozi wa sasa na wale wa zamani," alisema Msolla.

Kuhusu sakata la wachezaji Lamine Moro, Metacha Mnata na Michael Sarpong, Msolla alisema nyota hao wote walikuwa nje ya timu kutokana na masuala ya utovu wa nidhamu hivyo kurejea kwao kunatokana na kile kilichojadiliwa baina yao na kamati ya nidhamu.

"Metacha hakuna asiyejua alichofanya alianzia Dodoma, akafanya hivyo tena katika Uwanja wa Benjamini Mkapa, Moro aliondolewa tulipokuwa Mtwara pia kutokana na utovu wa nidhamu nilishangaa kumuona juzi kambini, hivyo hivyo kwa Sarpong naye aliondolewa kikosini kutokana na nidhamu.

"Mwalimu tuliye naye anazingatia sana suala la nidhamu ndio maana unaona hivi sijui kwa mwalimu aliyepita lakini hata mimi ni muumini wa nidhamu waulize wachezaji waliopita chini yangu hata uwe na kipaji kama huna nidhamu huwezi kupata nafasi, " alisema Msolla.

Msolla alitoa shukrani zake kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu suala la kuondolewa kodi kwa nyasi bandia na kwamba jambo hilo litasaidia kukuza mchezo wa soka, lakini amemuomba apunguze pia gharama za vifaa vya michezo.

Chanzo: www.habarileo.co.tz