Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msolla apewa mchongo mpya Yanga

56049 Pic+msolla

Tue, 7 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Dk Mshindo Msolla amepewa mbinu tano ambazo zitampa mafanikio katika uongozi wake wa miaka minne atakaokuwa madarakani.

Wanachama 1,276 walimchagua Dk Msolla kuwa mwenyekiti mpya wa Yanga katika uchaguzi mkuu uliofanyika juzi kwenye Ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi Oysterbay, Dar es Salaam.

Muda mfupi baada ya kutangazwa mshindi, Dk Msolla alisema kipambele chake cha kwanza ni kuondoa makundi na alitaka kambi zote zilizojitokeza wakati wa uchaguzi kuungana kujenga Yanga mpya.

Pamoja na mikakati ya Dk Msolla, wadau wa michezo wametoa maoni tofauti kwa mwenyekiti huyo wakimtaka kusimamia vyema mapato na mambo mengine ya kiutawala.

Mchambuzi Ally Mayay alisema jambo la kwanza analotakiwa kufanya Dk Msolla ni kubuni vyanzo vipya vya mapato ambavyo vitampa fursa ya kuijenga Yanga imara itakayokuwa na wachezaji bora wenye uwezo wa kushindana.

“Klabu ikiwa na fedha kila kitu kinawezekana, itasajili wachezaji wazuri, itaajiri kocha mzuri itajenga uwanja italipa mishahara na mambo mengi yatafanyika kwa mafanikio,” alisema nahodha huyo wa zamani wa Yanga.

Mayay alisema hatua ya wadau wa klabu hiyo kuchangishana fedha inayoendelea katika maeneo mbalimbali nchini, inapaswa kusitishwa ili kumpa nafasi Dk Msolla kutafakari namna ya kuiendesha Yanga kibiashara.

Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi alisema Dk Msolla anatakiwa kuongeza idadi ya wanachama.

Bayi alisema uongozi una wajibu wa kubuni mkakati wa kukusanya fedha kupitia wanachama ambazo zitatumika kwa maendeleo ya klabu.

“Klabu inaweza kuwa na mashabiki wengi, lakini hawamsadii Dk Msolla na timu yake. Ni vyema watoe fursa kwa mashabiki kuwa wanachama na fedha watakazochangia zitasaidia mambo mbalimbali ya klabu,” alisema mwanariadha huyo nyota wa zamani wa kimataifa.

Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Tarimba Abbas alisema Dk Msolla ana kazi ya kuvunja makundi na kuijenga Yanga kuwa na umoja na mshikamano.

“Yanga ilikuwa vipande vipande ilipoteza mwelekeo naamini uongozi ulioingia madarakani utaiweka Yanga katika mstari,” alisema Tarimba.

Kwa upande wake Mwenyekiti Mstaafu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Kanali Idd Kipingu alisema uongozi unapaswa kujipanga kujua namna bora ya kuongeza mapato kwa klabu.

Mbali na Msolla aliyemshinda Dk Jonas Tiboroha aliyepata kura 60 katika uchaguzi huo, viongozi wengine waliochaguliwa ni Frederick Mwakalebela (makamu mwenyekiti) na wajumbe ni Hamad Islam, Dominick Ikute na Frank Kamugisha.

Wajumbe wengine ni Saad Khimji, Salim Rupia, Rogers Gumbo, Arafat Haji na Bahati Mwaseba.



Chanzo: mwananchi.co.tz