Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mrithi wa Yondani Stars huyu hapa

16118 Pic+yondani TanzaniaWeb

Fri, 7 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Uwepo wa beki Aggrey Morris katika kikosi cha Taifa Stars kitakachocheza na Uganda kesho kwenye mechi ya kuwania kufuzu Fainali za Afrika (Afcon), unaondoa presha ya kukosekana kwa beki nguli Kelvin Yondani aliyeumia.

Majeraha ya goti ambayo Yondani amepata siku mbili kabla ya safari ya Uganda, yamemfanya akose mchezo huo muhimu wa ugenini utakaochezwa kwenye Uwanja wa Namboole jijini Kampala.

Uzoefu na kiwango bora cha nahodha huyo wa Yanga, kimemfanya kuwa chaguo la kwanza katika nafasi ya beki wa kati kwenye kikosi cha Taifa Stars na ilitarajiwa aanze na mchezaji wa Baroka, Abdi Banda katika mchezo huo wa kuwania kufuzu Afcon mwakani nchini Cameroon.

Ingawa kikosi cha wachezaji 23 wa Taifa Stars kilichosafiri jana kwenda Uganda kina mabeki wa kati watano, Morris ndiye anayepewa nafasi ya kuanza na Banda katika nafasi ya mabeki wa kati kuziba pengo la Yondani.

Sababu inayombeba Morris dhidi ya mabeki Ally Abdulkarim, David Mwantika na Andrew Vincent ‘Dante’ ni uzoefu wake katika mechi za ushindani alizocheza akiwa na Taifa Stars na klabu yake ya Azam kulinganisha na wenzake.

Morris ameitumikia Taifa Stars kwa nyakati tofauti ndani ya kipindi cha miaka minane, tangu alipoanza kuitumikia kwa mara ya kwanza mwaka 2010.

Rekodi hiyo inamfanya Morris kuwa ndio mchezaji aliyeitumikia Taifa Stars kwa muda mrefu zaidi katika kikosi kilichokwenda Uganda ingawa pia uwezo wake ndani ya uwanja ni kigezo kingine kinachomfanya kuwa mbadala sahihi wa Yondani.

Lakini pia beki huyo amekuwa chaguo la kwanza kwenye kikosi cha Azam kwa miaka tisa mfululizo tangu aliposajiliwa akitokea Mafunzo ya Zanzibar mwaka 2009.

Morris kama ilivyokuwa kwa Yondani, ana uwezo mkubwa wa kuruka kupiga mipira ya vichwa na kuokoa mashambulizi yatokanayo na mipira ya krosi au kona, stamina ya kutosha kukabiliana na washambuliaji wanaotumia nguvu pia amekuwa akiipanga vyema timu inapojilinda.

Beki na nahodha huyo wa Azam mbali na sifa hizo, amekuwa na uwezo wa hali ya juu wa kufunga mabao na upigaji wa mikwaju ya faulo na penalti, jambo ambalo linaweza kumpa ushawishi wa ziada Kocha wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike ili ampe nafasi kwenye kikosi cha kwanza.

Hata hivyo, pengo kubwa la Yondani linaweza kuwa ni kukosa maelewano baina ya Banda na Morris kutokana na wawili hao kutowahi kucheza pamoja kwenye kikosi cha Taifa Stars kama ilivyokuwa kwa beki huyo wa Yanga na Banda.

Tatizo jingine linaloweza kuiweka kwenye wakati mgumu Taifa Stars kwa kumkosa Yondani, ni Morris na Banda wote kutokuwa na kasi kutokana na asili ya maumbo yao huku wakiwa wanakutana na washambuliaji wa Uganda wanaosifika kwa kushambulia kwa kasi na uwezo mkubwa wa kupiga chenga.

Kocha msaidizi wa Azam, Idd Nassor ‘Cheche’ aliliambia gazeti hili kukosekana Yondani hakuna uhusiano na aina yoyote na matokeo yatakayopatikana kwenye mchezo huo.

“Kocha ndio kwanza ameanza kazi na hajakaa na wachezaji muda mrefu. Matokeo ya mchezo kwa kiasi kikubwa yanachangiwa na kiwango na ubora wa maandalizi ambayo timu imefanya.

Timu yetu imefanya maandalizi muda mfupi kulinganisha na wenzetu, kiuhalisia mechi itakuwa ngumu kwetu hata kama Yondani angekuwepo,” alisema Cheche.

Amunike alisema Yondani alikuwa katika mpango wake, lakini yupo mchezaji wa kuziba pengo lake kwa kuwa ana kikosi kipana hasa katika safu ya ulinzi.

“Yondani kama nilivyowahi kusema ameachwa sababu ni mgonjwa, yeye pamoja na Ngalema (Paul), lakini narudia tena nina kikosi kipana chenye uwezo wa kufanya vizuri katika mchezo wetu na kutupa matokeo,” alisema kocha huyo muda mfupi kabla ya wachezaji wa Taifa Stars kwenda Uganda.

Chanzo: mwananchi.co.tz