WAKATI Kocha wa Namungo Hemed Morocco akisema kuwa anahitaji muda kuifanya timu yake kuwa tishio baada ya kuanza upya kutokana na usajili mkubwa walioufanya, straika wake David Molinga ‘Falcao’ amekiri kuwa ana kazi ya kufanya ili kufunga mabao zaidi ya 10 msimu huu.
Namungo imecheza mechi nne ikishinda moja, imefungwa moja na kutoka sare mbili ilianza na Geita 2-0, ilifungwa na Azam FC 1-0, na imetoka sare na KMC bao na Kagera Sugar zote zikifungana 1-1.
Akizungumza na Mwanaspoti, Morocco alikiri kuwa na mwanzo mbaya na kuweka wazi kuwa sababu ya ni kutokana na kukosa kikosi cha kwanza baada ya kufanya usajili wa nyota wengi wapya.
“Ninahitaji muda ili niweze kutengeneza kikosi ambacho kinaweza kunipa matokeo ya haraka. Hadi sasa nasuasua kutengeneza kikosi cha kwanza siwezi kuwa na matokeo mazuri kwa haraka,” alisema.
“Usajili nimeufanya mwenyewe na ni mzuri. Nina wachezaji wengi wazoefu na wanajua mpira, lakini bado hawajawa na muunganiko. Naamini nikipata muunganiko nitakuwa bora na muda bado nina imani ya kuwa bora kadri muda unavyozidi kwenda.”
Kocha huyo alisema mbali na kukosa matokeo kwa kutokuwa na muunganiko, ligi ya msimu huu ni ngumu na itakuwa bora kutokana na mipango ya kila timu mwanzoni mwa msimu kuvuna ilichopata kutokana na maandalizi iliyoyafanya.
Kwa upande wake, Molinga ambaye aliwahi kuichezea Yanga, aliyejiunga na timu hiyo msimu huu alisema: “Namungo ni timu nzuri na imefanya usajili mzuri. Nimekutana na nyota wengi wazuri, natarajia msimu mzuri na bora ndani ya hii timu. Changamoto ni ugumu wa ligi na mipango ni kufunga mabao zaidi ya 10.
“Sijawahi kumhofia mchezaji yeyote kwenye kila timu niliyowahi kucheza, naamini kwenye kipaji na uwezo nilionao.”