Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkwasa: Refa ndiye sababu ya ushindi wa Yanga

12944 Pic+mkwasa Mkwasa: Nyota wa mechi Yanga ni refa

Thu, 4 Nov 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

BAADA ya kushuhudia Yanga ikitokea nyuma kwa bao 1-0 na kushinda 3-1 kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa juzi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Kocha Mkuu wa Ruvu Shooting, Boniface Mkwasa, ameulalamikia uchezeshaji wa mwamuzi Emmanuel Mwandembwa wa Arusha, kuwa chanzo cha kipigo hicho kutokana na maamuzi yake ya kuwakandamiza.

Akizungumza baada ya mechi hiyo ya Ligi Kuu Tanzania Bara, Mkwasa alisema kuwa kila mwenye macho ameona na mwamuzi huyo ndiye aliyekuwa nyota wa mchezo huo ('Man of the Match' ) kwa kufanya matukio kadhaa ya kuwatoa wachezaji wake mchezoni.

"Kila mtu aliona kilichotokea, kwa sababu tuliingia na mpango mkakati ambao ulikuwa umekaa vizuri, lakini mwamuzi aliamua kututoa kwenye mchezo, naheshimu maamuzi, lakini kwenye mechi hii 'Man of the Match' (Nyota wa Mchezo) alikuwa mwamuzi kwa kuwatoa wachezaji wangu kwenye morali," alisema kocha huyo wa zamani wa Yanga.

Matukio ambayo Ruvu Shooting wamekuwa wakilalamikia ni kutolewa kwa kadi nyekundu beki wao, Santos Mazengo, pamoja na penalti ambayo picha za marudio zinaonyesha kuwa mpira huo ulishikwa na mshambuliaji wa Yanga, Fiston Mayele na mwamuzi aliamuru 'tuta', huku akimwonya kwa kadi ya njano beki Ally Mtoni 'Sonso' kwa madai kuwa ndiye aliyeunawa.

Hata hivyo, Mkwasa alisema kuwa timu yake haikucheza vibaya, ni kwa sababu tu walikuwa pungufu kwa mchezaji mmoja kwa muda mrefu.

"Yanga walikuwa na faida ya kuwa na mtu mmoja zaidi, na kwa sababu wana uwezo wa kukaa na mpira na sisi muda mrefu tunautafuta, ilisababisha wachezaji wangu kuchoka," alisema.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela, alisema kikosi chao kinaonyesha kuwa kinaendelea kubadilika kila kukicha, kwani pamoja na kutanguliwa bao, lakini hawakuhamaki.

"Wachezaji walitulia na kuweza kurudisha goli na kupata mengine ya ushindi," alisema Mwalalebela ambaye amekiri ugumu wa Ligi Kuu msimu huu.

"Ni msimu mgumu kwa sababu timu nyingi zimeleta wachezaji vijana wenye uwezo mkubwa wa kupambana, tumeona matokeo mengine ya kikatili kama wenzetu wanapambana sana, lakini mwisho wa siku hawapati matokeo na hii ni kulishukuru Shirikisho la Soka nchini (TFF) kwa kuifanya ligi kuwa bora kutokana na udhamini," alisema Mwakalebela.

Yanga imefikisha pointi 15, ikiwa kileleni, Ruvu Shooting ikiwa na pointi sita kwa timu hizo kila moja kushuka dimbani mara tano.

Kwa sasa ligi hiyo inaelekea mapumziko kupisha Kalenda ya Fifa ya mechi za kuwania kufuzu Kombe la Dunia mwakani nchini Qatar, ambapo kwa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars itaikaribisha DR Congo Alhamisi ijayo katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kabla ya Jumapili ya Novemba 14, mwaka huu kushuka dimbani nchini Madagascar kuwavaa wenyeji hao.

Ligi hiyo itarejea tena Novemba 19, kwa Ruvu Shooting kuikaribisha Simba wakati kesho yake Yanga wakiwa wageni wa Namungo FC walioshuka Uwanja wa Mkapa jana dhidi ya 'Wekundu wa Msimbazi'.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live