NYOTA wa zamani wa Yanga, Charles Bonifasi Mkwasa na Herry Morris, wametoa neno kuwa ili timu hiyo ishinde mchezo ujao na kusonga mbele inapaswa kufanya maandalizi ya hali ya juu pamoja na kutumia kila nafasi itakayopatikana katika mchezo wa marudiano utakaofanyika Septemba 19, katika Uwanja wa Yakubu Gowon nchini Nigeria.
Yanga inashuka dimbani katika mchezo huo ikiwa nyuma kwa bao 1-0, baada ya kuteleza na kupoteza katika mchezo wa kwanza uliofanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Akizungumza jana, Mkwasa, alisema kuwa Yanga, inakabiliwa na mchezo mgumu unaohitaji matokeo ya ushindi ili iweze kusonga mbele na itawezekana kama umakini utaongezeka hasa katika safu ya ulinzi ipunguze makosa na safu ya ushambuliaji itumie kila nafasi itakayopatikana.
“Bado kuna nafasi kwao ya kusonga mbele ila wanapaswa kufanya kazi kubwa lakini kama watatulia na kuhakikisha wanatumia kila nafasi wanayoipata naamini hilo litazaa matunda, Yanga itashinda.” alisema Mkwasa.
Naye mshambuliaji wa zamani Morris, alisema kuwa ni wakati wa kila mchezaji kujituma na kuisaidia timu kwa kufunga pale nafasi inapopatikana sio kumtegemea mchezaji mmoja pekee lakini pia kocha Nassredine Nabi, asimtwishe mzigo mkubwa Heritier Makambo.
“Kocha Nabi, asimtegemee Makambo pekee pale mbele, kama itawezekana katika mchezo ujao aanzishe washambuliaji wawili naamini kama atafanya hivyo tutapata matokeo na kusonga mbele.” Alisema Morris.