Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkwabi avunja ukimya uwekezaji wa Mo’ Simba SC

68467 Nkwabi+pic

Sun, 28 Jul 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Siku chache baada ya Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe kutoa muongozo wa uwekezaji kwenye klabu za soka zilizoanzishwa na wanachama, Rais wa Simba, Swedi Mkwabi amevunja ukimya kuhusu hatma ya mwekezaji wa klabu hiyo, Mohammed ‘Mo’Dewji.

Simba ni klabu ya kwanza nchini iliyoanzishwa na wananchi kuingia kwenye mfumo wa uendeshaji wa hisa ambapo katika mchakato huo ilimpa mwekezaji wao, Mo’ Dewji asilimia 49 na wanachama kubaki na asilimia 51.

Hata hivyo, Jumatano Waziri Mwakyembe alitoa muongozo wa uwekezaji katika klabu za soka zilizoanzishwa na wanachama akisisitiza kuwa asilimia 49 za hisa si za mwekezaji mmoja bali watatu nakuendelea.

Katika muongozo huo, Waziri Mwakyembe alisema baada ya kubadili kanuni za Baraza la Michezo la Taifa (BMT), wanachama watabaki na asilimia 51 na wawekezaji kuanzia watatu au zaidi watagawana asilimia 49 ya hisa na si zote 49 kuhodhiwa na mtu mmoja.

Kauli hiyo ni kama inaiweka mtegoni Simba ambayo tayari ilikuwa imetoa asilimia 49 kwa Mo’ katika mchakato ulioanza mwaka 2018.

Nukuu ya Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa (Sura ya 49) inasema:

Pia Soma

“Kwa mujibu wa Kanuni za Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa (Marekebisho) ya mwaka 2017 ambazo zinasomwa pamoja na Kanuni za Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa, za mwaka 1999, ambazo katika Kanuni hizo zitaitwa Kanuni Kuu.

“Kanuni Kuu zinarekebishwa kwa kuongeza mara baada ta Kanuni ya 18, Kanuni mpya ya 18A kama ifuatavyo: 18A - (1) Vyama au vilabu vya michezo vilivyoanzishwa na wanachama vikiamua kuuza hisa zake vinapaswa kutenga asilimia hamsini na moja kwa ajili ya wanachama wake na asilimia arobaini na tisa kwa wanaotaka kununua.” Mwisho wa kunukuu.

Neno la mwisho katika kifungu la “wanaotaka kununua” na si “anayetaka kununua” ndilo linalotajwa kuwa msumari wa moto katika mpango wa Mo’ kumiliki asilimia zote 49.

Akizungumzia hatma ya Dewji ndani ya klabu hiyo, na msimamo wa klabu ya Simba baada ya agizo la Waziri Mwakyembe, Rais wa Simba, Mkwabi alisema ni jambo zito ambalo linahitaji majadiliano mapana.

“Ni jambo zito ambalo binafsi nimelisikia kupitia vyombo vya habari, sikuwepo nchini kwa siku kadhaa, hivyo sijui likoje, lakini nimelisikia pia,” alisema.

Bosi huyo wa Simba alisema muongozo huo unahitaji majadiliano mapana ya Bodi ya Wakurugenzi wa Simba kabla ya kutoa majibu ya nini watafanya.

Alisema pamoja na tamko hilo la Serikali, hakuna kitakachoharibika baada ya uongozi wa Bodi kukaa na kujadili suala hilo kwa upana.

Mchakato wa Simba kuelekea kwenye mabadiliko ya uendeshaji wa klabu ulionekana kupingwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa klabu hiyo, Hamis Kilomoni ambaye hivi karibuni, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba Crescentius Magori alimtangaza kuwa si mdhamini wao tangu Novemba 2017.

Magori alisema tayari klabu imepata hati mpya ya mali za klabu hiyo baada ya kutangaza ile ya awali ambayo anayo Kilomoni imepotea huku akisisitiza kuwa Kilomoni hawezi kukwamisha mchakato wa mabadiliko ya uendeshaji wa hisa ndani ya klabu hiyo.

Chanzo: mwananchi.co.tz