Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mkurugenzi Temeke kuufunga Uwanja wa Taifa, Azam Complex

50325 Pic+taifa

Thu, 4 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Halmashauri ya Manispaa ya Temeke imetangaza dhamira ya kuvifungia viwanja vya Uwanja wa Taifa, Azam Compex na viwanja vya Maonyesho vya Sabasaba kwa kuwa wamiliki wa viwanja hivyo hawajawahi kulipa kodi ya ushuru wa huduma tangu  vijengwe.

Akizungumza Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Lusubilo Mwakibibi amesema kuanzia jana wamiliki wa viwanja vya Uwanja wa Taifa na Azam Compex watafute viwanja vingine vya kuchezesha mechi ambazo wanazo kuanzia sasa kama hawatalipa kodi hiyo.

Mwakibibi alisema kodi ya ushuru wa huduma hiyo wanayohitaji halmashauri ya manispaa hiyo ni asilimia 0.3 ya mapato wanayoingiza kila uwanja unapotumika .

"Hatuwezi kuendelea na utaratibu huu mfano sasa hivi kuna maandalizi ya sabasaba katika viwanja vya maonyesho vya Sabasaba  pamoja na viwanja vya uwanja wa Taifa na Azam Compex kuna mechi zinaendelea ninawatuma watu wetu  waje kuzuia  kwenye milango kisifanyike kitu chochote hadi hapo mtakapolipa kodi ya ushuru wa huduma,"alisema Mwakibibi.

Alisema akishawaandikia barua tangu mwaka 2018 wawe wameshalipa kodi hiyo ifikapo Aprili Mosi lakini hakuna hata mmiliki wa viwanja hivyo aliyeenda kulipa kodi hiyo.

Mwakibibi alitolea mfano wa Uwanja wa Taifa walipowakumbusha wamekuwa wakipiga danadana mara  wanaohusika ni Serikali Kuu mara ni Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) .Pia upande wa Azam Complex walionyesha nia ya kulipa lakini  wamekuwa wakiwazungusha bila mafanikio.

 

Na upande wa viwanja vya Maonyesho vya Sabasaba wao walionyesha nia ya kufanya mazungumzo lakini baadaye waliieleza halmashauri hiyo anayetakiwa kuzungumza hayupo.

Alisema kinachohitajika wamiliki wa viwanja hivyo walipe kodi wakumbuke hivi karibuni ilichezwa timu ya taifa ya Uganda na Tanzania watu walijaa hadi nje ya uwanja watu walitupa ovyo uchafu kazi ya halmashauri ni kusafisha lakini hawakupewa fedha ya kodi ya ushuru wa huduma.

Mwakibibi alisema wanapokusanya kodi hiyo inasaidia kuwalipa watu wanaofanya usafi pembezoni mwa barabara za halmashauri hiyo na pia wana uhaba wa vyumba vya madarasa hivyo  fedha hizo zitasaidia kujenga madarasa 140.



Chanzo: mwananchi.co.tz