Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mitambo mipya Simba SC yajibu kwa kishindo

10475 MITAMBO.png TanzaniaWeb

Sun, 1 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mabingwa wa kihistoria wa Kombe la Kagame, Simba imejaribisha mitambo yake na imekubali.

Simba ilikuwa katika pilika za usajili wa wachezaji wapya na imepanga kutumia michuano ya Kagame kujaribisha vifaa vyake.

Mambo yameonekana jana baada ya mastaa wake wapya kuanza kwa kishindo michuano hiyo kwa kuitandika Dakadaha ya Somalia mabao 4-0.

Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini, wachezaji wake wapya, Marcel Kaheza, Adam Salamba na Rashid Juma ndiyo walioitia njaa Dakadaha.

Bao la kwanza la Simba liliwekwa kimiani katika dakika ya 15 ya mchezo na Kaheza kwa mkwaju wa penalti baada ya Abbas Amin Mohammed kuunawa mpira akiwa ndani ya eneo la hatari. Kaheza alisajiliwa na Simba akitokea Majimaji ya Songea.

Kuingia kwa bao hilo kuliwafanya washambuliaji wa Simba kuongeza kasi ya mashambuzi na juhudi zao zikazaa matunda katika dakika 23 walipoongeza bao la pili likifungwa na Adam Salamba akipokea pasi safi kutoka kwa Ally Shomari.

Mabao hayo yaliwafanya Dakadaha kupoteza mwelekeo wakiacha kabisa kushambulia na kurudi langoni mwao ‘kupaki basi’ jambo lililokaribisha mashambulizi mengi ya Simba.

Hata hivyo, mbinu hizo ziliwasaidia kupunguza idadi ya mabao, kwani ilibidi Simba wasubiri hadi dakika ya 45 kupata bao la tatu lililotokana na kazi nzuri iliyofanywa na kiungo mzoefu Mwinyi Kazimoto aliyetengenezea Rashid Juma naye bila ajizi aliukwamisha mpira nyavuni kuipeleka Simba mapumziko ikiongoza kwa mabao 3-0.

Kipindi cha pili Simba iliendelea kusaka mabao hata hivyo mtindo wa Dakadaha kujilinda ulionekana kufanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani waliwalazimu wachezaji wa Simba kuamua kupiga mashuti ya mbali ambayo hayakuwa na manufaa.

Simba ilipata bao la nne katika dakika ya 76 likifungwa na Salamba tena, baada ya kuachia shuti kali akiwa nje ya 18, baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Kazimoto. Salamba kajiunga Simba akitokea Lipuli ya Iringa. Kocha msaidizi wa Simba, Masoud Djuma, alifanya mabadiliko kwa kumpumzisha Kaheza katika dakika ya 79 akimuingiza Said Ndemla, hata hivyo mabadiliko hayo hayakusaidia kubadilisha matokeo, hivyo hadi mwisho Simba 4-0 Dakadaha.

Katika mechi za ufunguzi wa michuano hiyo iliyopigwa juzi, Azam FC waliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Kator ya Sudan Kusini, mabao ya Azam yakifungwa na Shaaban Idd bao la Kator likifungwa na Jimmy Nahari.

Mchezo mwingine ulimalizika kwa Singida United inayoshiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza kuizamisha ya APR ya Rwanda kwa mabao 2-1, mabao yake yakifungwa na Habib Kyombo na John Tibar.

Michuano hiyo inaendelea leo kwa Rayon ya Rwanda kukipiga na Gor Mahia ya Kenya mchezo utakaoanza saa 8:00 mchana kwenye Uwanja wa Taifa wakati mchezo wa pili ukipigwa saa 10:00 jioni kati ya JKU ya Zanzibar dhidi ya Kator FC ya Sudan Kusini kwenye uwanja wa Chamazi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.

 

Chanzo: mwananchi.co.tz