Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Miraji amfunika Kagere Simba ikirejea kileleni

85642 Pic+miraj Miraji amfunika Kagere Simba ikirejea kileleni

Sun, 24 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba SC jana walirejea katika uongozi wa ligi hiyo ikiwa ni saa 24 tangu walipoondolewa na Kagera Sugar juzi, baada ya kuifunga Ruvu Shooting mabao 3-0 katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Juzi, Kagera Sugar ilikalia kiti cha uongozi baada ya kuifunga Lipuli FC mabao 2-1 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba na hivyo kufikisha pointi 23 dhidi ya 22 ilizokuwa nazo Simba.

Hata hivyo, mabao matatu yaliyofungwa na kiungo Miraji Athuman (mawili) na beki Mbrazil Tairone Santos yalitosha kuwatoa kileleni Kagera Sugar baada ya Simba kufikisha pointi 25. Katika ushindi huo Miraj alifunga kwenye dakika za 39 na 74 huku Traore akifunga kwa kichwa katika dakika ya 47.

Licha ya ushindi huo, mshambuliaji wa Simba anayeongoza kwa mabao Meddie Kagere hakufunga bao katika mchezo ukiwa ni wa tatu kwake kutofumania nyavu tangu ligi ianze. Kagere ana mabao manane akifuatiwa na Paul Nonga wa Lipuli mwenye mabao saba huku Miraji (Simba) na Daruesh Saliboko (Lipuli) wamezimania nyavu mara sita.

Miraji alifunga bao la kwanza kwa kichwa akimalizia krosi ya Shomari Kapombe ambaye naye alipokea pasi nzuri kutoka katikati ya uwanja iliyopigwa na Hassan Dilunga.

Simba ilikwenda mapumziko ikiongoza kwa bao 1-0, lakini dakika mbili baada ya kipindi cha pili kuanza Tairone alifunga kwa kichwa kufuatia kona iliyopigwa na Francis Kahata.

Kahata pia alichangia bao la tatu ambapo alimpasia mfungaji, Miraji aliyeutumbukiza mpira wavuni.

Aussems awapagawisha mashabiki

Kocha wa Simba, Patrick Aussems aliuteka uwanja alipoingia, baada ya mashabiki wa timu hiyo kumshangilia kwa nguvu.

Aussems yupo kwenye wakati mgumu na mabosi wake kutokana na kumtuhumu kuondoka nchini kwenda Afrika Kusini bila idhini jambo linalotishia kibarua chake.

Hata hivyo, jana wakati anaingia uwanjani alipokea mapokezi ya nguvu kutoka kwa mashabiki, pengine ikiwa ni majibu kwa uongozi kuwa bado wanamhitaji aendelee kukinoa kikosi chao.

Hali hiyo iliendelea hata baada ya mchezo na kujikuta akipewa ulinzi wa polisi baada ya mashabiki waliokuwa wakimshangilia kutaka kumkumbatia, huku baadhi yao wakiimba, “tunakupenda Uchebe hata kama viongozi hawakutaki”. Kocha huyo alisindikizwa na askari hao mpaka alipoingia kwenye gari la timu.

Chanzo: mwananchi.co.tz