Dar es Salaam. Wakati siku tatu zikipita tangu dirisha dogo la usajili lifungwe, kundi kubwa la wachezaji waliohama timu moja kwenda nyingine wameondoka baada ya kuvunja mikataba na klabu zao.
Ingawa mara kwa mara nyota wengi wanaofanyiwa uhamisho kwenye dirisha dogo huwa ni wale wanaotolewa kwa mkopo, huru au wale ambao klabu zao hukubaliana, mambo yamekuwa tofauti kipindi hiki kwani idadi kubwa ya wachezaji wamevunja mikataba yao na kwenda kwingine.
Sababu kuu ambayo inaonekana kuchangiwa na madai ya malimbikizo ya stahiki ambazo kundi kubwa la nyota hao walikuwa wanadai kwenye klabu walizotoka huku wakihisi kuna uwezekano finyu wa kulipwa.
Hali ya ukata ambayo imezikumba klabu nyingi za Ligi Kuu msimu huu ndio inaonekana imekuwa chanzo cha kuziumiza idadi kubwa ya timu za ligi hiyo jambo lililosababisha ziwapoteze nyota wao kirahisi.
Singida United ndio iliyoathirika zaidi kwa kuondokewa na wachezaji wake wengi kwani jumla ya nyota saba wamevunja mkataba na timu hiyo na kutimkia kwingine.
Mshambuliaji Elinyweshia Sumbi ametimkia Kagera Sugar, Salum Chuku ametua KMC, Miraji Adam amekimbilia Coastal Union, Eliuter Mpepo yupo Buildcon inayoshiriki Ligi Kuu ya Zambia, Shaffiq Batambuze amekwenda Gor Mahia, Manyika Peter na Jamal Mwambeleko wametimkia zao KCB ya Kenya.
Nyota hao wamevunja mikataba na Singida United kutokana na kile wanachodai kutolipwa stahiki zao za mishahara na ada ya usajili.
Ukiondoa Singida United, African Lyon nayo imekimbiwa na Adam Omary, Awadh Salum na Augustino Samson ambao wamevunja mikataba na klabu hiyo kwa sababu za kifedha.
Wengine waliovunja mikataba na timu zao kwa sababu za kifedha ni Bigirimana Blaise na Erick Mlilo ambao wameikimbia Stand United na kujiunga na Mbao FC na Alliance sawa na mshambuliaji Songa Bethel wa Biashara United ambaye ametua Alliance.
Upande wa Mbeya City, nyota wake wawili wa kikosi cha kwanza, Haruna Shamte na Babu Ally nao wameamua kuikimbia timu hiyo kutokana na kutolipwa madai yao. Martin Ilamfya naye ameachana na Mwadui na kutua zake KMC.
Mtendaji Mkuu wa Singida United, Festo Sanga alisema timu yake imewaruhusu bila kinyongo nyota wake saba kutimka kwa sababu wanafuata maslahi mazuri huko wanakoenda.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wilfred Kidao alisema kuwa kamati ya sheria na hadhi za wachezaji itakutana kujadili usajili wa dirisha dogo.
“Kamati itaketi muda sio mrefu na kupitia usajili wote wenye utata lakini wachezaji wote ambao usajili wao umefuata taratibu zote wamesharuhusiwa kuzitumikia timu zao walizoenda.”