Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Michezo yathibitisha kuvunja tofauti zetu

48948 Pic+michezo

Wed, 27 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Siasa ina nguvu kubwa katika mustakabali wa maisha ya kila siku ya binadamu.

Hivyo ni vigumu kutenga maisha ya kila siku na siasa kwani wanasiasa ndio hutoa mwongozo wa mambo mengi katika jamii.

Ndio sababu taifa lolote linapokuwa na siasa safi basi utawaona wananchi wake wana maendeleo.

Pia taifa linapokuwa na siasa safi ni wazi uchumi wake utapaa kwani wananchi watashiriki shughuli za kiuchumi bila hofu ya juu ya hatma ya mavuno yao.

Lakini taifa ambalo siasa zake zinayumba ni nadra sana kuona mafanikio katika shughuli za kiuchumi.

Taifa ambalo siasa zake zina tatizo, wananchi hupoteza furaha na shughuli nyingi za kiuchumi husimama na migogoro hukithiri.

Kutokana na umuhimu wa siasa bora katika jamii ndiyo sababu mataifa mengi yanaruhusu mitazamo tofauti katika siasa ili kuchochea maamuzi bora kwa wanasiasa.

Maamuzi bora yanapatikana kutokana ushindani wa mawazo ya wanasiasa hivyo wazo jema ndilo hupita na kutamalaki. Hali inapokuwa hivyo wananchi wanaweza kutofautiana kiitikadi na kimitazamo lakini wasiwe na wanapingana na kulumbana.

Naamini bado ni jambo bora kuruhusu mawazo mbadala ili kupata kilicho bora bila kujali tofauti za mitazamo yetu kiitikadi na hata kidini. Hivyo ni wazi kuwa tofauti za mitazamo ya kisiasa haziwezi kuwa ni uadui katika jamii miongoni mwa wanasiasa na jamii kwa ujumla kama ambavyo tumekuwa tukishuhudia.

Jambo ambalo linathibitishwa siasa sio uadui na ushiriki wa wanasiasa kwa pamoja katika masuala ya kijamii.

Miongoni mwa mambo ambayo yamethibitisha siasa si uadui ni ushiriki wa wanasiasa wote bila kujali tofauti za mitazamo katika michezo.

Baada ya miaka 39 Tanzania inarejea tena katika michuano ya mataifa ya Afrika na hili limechangia sana na umoja wa Watanzania wote.

Tumeshuhudia wanasiasa wa vyama vyote, wakihamasisha ushindi wa Taifa Stars na baadhi walifika uwanjani na kukaa pamoja.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliongoza umati wa Watanzania wakiwepo wafuasi wa vyama karibu vyote vya siasa, dinimbalimbali na viongozi wao uwanja wa Taifa kuishangilia Taifa Star.

Tukio hili linathibitisha kuwa tofauti zetu za kisiasa hazipaswi kutugombanisha, kutufanya maadui na kushindwa kuleta furaha kwa Watanzania.

Rais wa Jamhuri ya Muungano, John Magufuli katika mikutano yake kadhaa, amekuwa akizungumzia pia umuhimu wa ushiriki wa vyama vyote katika mambo muhimu katika jamii bila kujali itikadi zao. Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amethibitisha pia hili akiwa mjini Dodoma akizindua mkakati wa kukomaza demokrasia katika ngazi ya mashina.

Dk Bashiru anasema lazima vyama kuheshimiana kuacha matukio ya uhasama ikiwamo kuchoma bendera na akataka wana CCM kama chama tawala wanapoheshimu bendera za chama chao pia waheshimu na za wenzao na kuheshimiana.

Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa pia katika siku za karibuni, amethibitisha hili kuwa mitazamo ya kisiasa si uadui pale aliporejea CCM na kuipongeza Chadema, chama kikuu cha upinzani kilichompokea mwaka 2015.

Lakini pia kiongozi mkuu wa upinzani, Freeman Mbowe katika matamko yake kadhaa amekuwa akitoa kauli kuwa siasa ni majukwaa tu ya kuzungumza na wananchi na si uadui.

Hivyo kwa ujumla kilichofanywa na timu yetu ya Taifa kinaendelea kuthibitisha kuwa tunaweza kubaki na tofauti zetu za mitazamo ya kisiasa lakini Taifa likaendelea kuwa moja kuleta faraja kwa wengi.

Taifa Star inaifunga Uganda 3-0 uwanja wa Taifa na kwenda kushiriki michuano wa mataifa ya Afrika nchini, Misri hili linafanikiwa kutokana wanasiasa wetu wote kushirikiana.

Licha ya kwamba ushindani baina ya Simba na Yanga hupitiliza kiasi cha kuzinufaisha timu ngeni, lakini kikubwa ni kuwa mashabiki wa timu hizo huendelea kuheshimiana na kuchukulia hali hiyo kama utani wa jadi.

Naamini hii ndio Tanzania ambayo iliiacha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Tanzania moja ambayo mitazamo ya kisiasa haijawahi kuigawa na watu kuonana ni maadui.

Mussa Juma ni Mwandishi wa Mwananchi Mkoa wa Arusha 0754296503



Chanzo: mwananchi.co.tz