Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Michezo ya asili inavyonoga Zanzibar

Asili Znz Michezo ya asili inavyonoga Zanzibar

Sat, 4 Nov 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Kama sio Dk Hussein Mwinyi, mchezo wa makachu ambao ni wa asili ya Kizanzibar usingekuwa ni fursa ya ajira wa vijana.

Wenyeji wanasema, walirithi utamaduni wa kucheza makachu kutoka kwa babu, wajomba na kaka zao, ambao zamani walicheza kwa kujifurahisha, lakini sasa ndiyo ajira yao.

Huo ni mmoja kati ya michezo ya Kizanzibar ambayo inapendwa na watalii wanaotembelea kisiwa hicho hivi sasa.

Makachu hufanyika kwa staili, wanaocheza hudaivu baharini na kuogelea, lakini wanafanya wakiwa na picha, bendera au bango la mtu anayetaka kufanyiwa tangazo.

“Miaka ya nyuma makachu ilikuwa ni kama mchezo wa kujifurahisha, lakini sasa unatupa riziki, imekuwa ni ajira yetu,” anasema Daivan Smart ambaye ni miongoni mwa viogozi kwenye makundi ya mchezo huo.

Daivan ambaye jina lake halisi ni Ameer Suleiman Rashid anasema anahudumia familia yake kupitia makachu.

“Nilianza kucheze miaka minne iliyopita, wakati huo kulikuwa na changamoto nyingi, mwaka jana Rais wetu (Dk Hussein Mwinyi) alitutembelea kushuhudia mwenyewe namna tunavyo shiriki.”

DK MWINYI AUBORESHA

Anasema ziara hiyo ilitoa fursa nyingi, ikiwamo mchezo huo kusajiliwa na kutambulika na Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ).

“Alitusaidia kusafisha hili eneo wakatoa mawe makubwa ambayo yalikuwa ni hatari zaidi tunaporuka, katika miaka yake mitatu amekuja kuzungumza na sisi kujua changamoto zetu na huu mchezo umetambulika na serikali.

Anasema zaidi ya vijana 100 wanafanya makachu, wote wanapata riziki na Rais Mwinyi amewaahidi kuwaboreshea zaidi eneo hilo kwa kuwawekea ngazi za kutokea nchi kavu.

“Ni mchezo unaotupa riziki, japo sio kila siku tunapata, kuna nyakati hatuingizi chochote, lakini kuna siku neema inakuwepo, tunapata pesa,” anasema.

Akitolea mfano, anasema anapofanya matangazo anaingiza hadi Sh 400,000 na amefanya matangazo na wasanii wakubwa, TANAPA na tasisi nyingine tofauti.

“Malipo haya tunayapata kwa wageni, watu wa ndani (wenyeji) wanapenda kuomba kutulipa elfu 20 au elfu 40, wageni wao hutulipa vizuri,” anasema Daivan Smart.

Akimuelezea Rais Mwinyi, anasema alifika eneo hilo kuwatembelea, yeye Daivan kama kiongozi alizungumza naye kwa niaba ya wenzake.

“Alitusalimia vijana wake, akatwambia makachu ni kazi, akatuwekea mazingira rafiki ya kufanya kazi hii ikiwamo kutuondolea mawe ambayo zamani ili kuruka, unaweza kudondokea kwenye jiwe ukapata madhara.”

ATHARI ZA MAWE

Inaelezwa wapo waliowahi kupoteza maisha, wengine kuumia na madhara mengine kama hayo kutokana na kupiga mbizi kwenye mawe.

“Katika kupiga kachu, kuna watu wanataka water full (maji mengi) wengine wanataka maji madogo, na kwenye kachu huwezi kupiga kwenye mawe, tulifanya kiubishi, lakini Rias wetu alitusafishia sasa pamebaki mchanga na kutupa mazingira rafiki ya kufanyia kazi, vikundi vitano tayari vimesajiliwa kucheza makachu.

Anasema kila siku vijana wanazidi kuongezeka eneo hilo kucheza makachu, ingawa sasa wanataa kubadili utaratibu ili wachezaji wapya wazifuate sio mtu akijisikia anakwenda ‘kudaivu’ wakati wengine hawajui na wanahitaji wafundishwe kwanza.

Atoa fursa mpya kwa vijana Sameer ambaye alisomea ubaharia kabla ya kuingia kucheza makachu, anasema vijana wengi wametoka mtaani na kuingia kujishughulisha na makachu.

“Kuiba, kunyang’anya sio jambo zuri, hivyo vijana wanatoka mtaani na kuja hapa kutafuta riziki na wote tunapata, lakini pia tunaitangaza Zanzibar na Tanzania kupitia mchezo huu, watalii wengi wanakuja kuangalia, wanapenda na wanapotajwa wao na nchi zao wanafurahi na kutulipa,”.

Kabla ya usajili changamoto zilikuwa hivi

Sameer anasema walikuwa na changamoto ya kupata fomu namba tatu ya polisi (PF3), pale mwenzao anapoumia na kupelekwa hospitali.

“Ulikuwa ni mchezo ambao hautambuliki, nakumbuka huko nyuma kuna mwenzetu mmoja ‘alidaivu’ akazama, tulifanya juhudi kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu tukamuokoa tulikwenda kwa wazazi wake tukashirikiana nao hadi akapona.

“Mimi pia niliwahi kuruka taili ya hozara, wakati huo najifundisha, niliruka vibaya pumzi zikakata, lakini hizo zote ni changamoto za kawaida kama vinavyotokea kwenye kazi nyingine, sikuacha kucheza hadi leo.”

Mbali na hozara, kwenye makachu kuna staili nyingine kama kibaraza, fly, chempu mkato, chempu kachu, huku fly ikitajwa kuwa ni rahisi kujifundisha na hozara ni ngumu kidogo.

“Kuruka hozara unatakiwa kichwa kiangalie wawingu kisha ugeuke juu kwa juu kichwa chini miguu juu wakati unadaivu,” anasema.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar (BTMZ), Said Marine anasema mchezo huo ni maarufu visiwani huo kwa sasa.

“Umeanza kuchezwa miaka mingi, ulikuwa na changamoto zake, katika miaka mitatu ya Dk Mwinyi, tumeutengenezea mfumo mzuri na una sheria zake, matatizo yaliyokuwa yanatokea hatutaki yaendelee, suluhisho ikawa ni kuusajili na kuwa-control (kuwaongoza) washiriki.

“Kwenye sherehe za Mapinduzi msimu huu, makachu nayo itakuwepo, umekuwa ni kitega uchumi kwa vijana kujiajili na kupata kipato,” anasema.

Mchezaji mwingine, Mbarouk Salum Mbarouk mzaliwa wa Michenzani, ambaye ana uzoefu wa miaka minne kucheza makachu anasema katika miaka mitatu ya Dk Mwinyi kuna mabadiliko.

“Ulikuwa unachukuliwa kama mchezo wa hatari, lakini umechezwa na babu, baba, wajomba na kaka zetu miaka yote, sisi tumeurithi kwao, lakini Dk Mwinyi ndiye amekuwa Rais wa kwanza kufika eneo hili na kuona kuna fursa, akatuboreshea mazingira na sasa ni kivutio pia cha watalii.”

Mbarouk anasema makachu imempa pesa ya kuendesha maisha yake na kufanya vitu vingi, ingawa hakutaka kuviweka wazi akihofia jamii itakavyochukulia.

“Huku tunajua, naweza nikasema, ukashangaa kesho vijana wamejaa hapa, wakijua kuna pesa, lakini ukweli riziki hatukosi, ni mchezo unaoendesha maisha ya vijana wengi.”

Adil Omary Nasoro mkazi wa Shangani ambaye mbali na kucheza makachu pia anafanya kazi ya kupeleka wageni visiwani anasema amepata marafiki wengi wa ndani na nje ya nchi kwa kupiga makachu.

“Zamani tulikuwa tukisogea eneo hili kupiga makachu tunafukuzwa na kugombezwa, lakini sasa imekuwa ni tofauti sisi tunawapa nguvu wadogo zetu ili wafanye vizuri.”

Achana na ajira 300,000 ambazo aliahidi kuzitoa katika sekta mbalimbali, kwenye sanaa na utamaduni hamasa ya Dk Mwinyi imetengeneza ajira nyingine 1000 zisizo rasmi kwa Wazanzibar, wengi wakiwa vijana.

Unaambiwa ukitaka jambo lolote linoge watumie vijana, ndicho kilichotokea baada ya Dk Mwinyi kuwaongoza Wazanzibar 1000 walioshirikishwa katika filamu ya kimataifa ya Milele iliyofanywa visiwani humo kwa siku 30, kisha Dar es Salaam siku moja na Arusha siku tano.

“Uhuru aliowapa vijana kwenye sanaa na utamaduni, kumefungua vitu vingi, tunaitizama miaka mitano kwenye muhura wake wa kwanza tutakuwa mbali zaidi ya hapa tulipo,” anasema Dk Omary Abdallah Adam Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa, Sensa ya Filamu na Utamaduni Zanzibar ( BaSSFU).

Anasema katika vitu ambavyo wamejifunza kipindi hiki ni uwekezaji kwenye production, akitolea mfano Filamu ya Milele ambayo ilifanyika kwa ubora wa hali ya juu, iIlifanyikia huko Matemwe katika Visiwa vya Mnemba,

“Ni filamu ambayo ina maudhui kama ya Royal Tour, Rais wetu pia alishiriki, iitazinduiwa Oktoba 31 kwa Lugha ya Kichina, kisha baadaye itazinduliwa kwa lugha ya kimataifa, hii imetupa somo la uwekezaji, Wachina walikuja na crew ya watu 150 ambao walikaa Zanzibar siku 30 na kutuingizia fedha za kigeni na kutufundisha pia kuhusu production, achilia mbali Wazanzibar 1000 walioshirikishwa katika maeneo mbalimbali.

Anasema ili kuboresha kazi za wasanii, katika kipindi chake alishauri kuwepo mfuko wa wasanii ambao huko katika hatua za mwishoni kukamilika na tayari jukwaa hilo linashirikisho vyama 13 vimejisajili ili kufanya kwa wepesi kazi zao tofauti na miaka ya nyuma walikuwa wametawanyika.

“Imetoa fursa nyingine kuna watu wamejitokeza kutaka kujenga studio kubwa ya filamu hapa Zanzibar, kama haitoshi kwenye wilaya zetu 11 kuna mkakati wa kukusanya 300milioni kwenye sekta ya utamaduni,” anasema.

URITHI WA NGOMA

Anasema katika Mapinduzi ya 1964 wananchi walikutana zaidi kwenye fete (bonanza) huko ndiko mipango mingi ilipangwa.

“Ngoma za asili ni urithi wetu na katika sherehe za kumbukumbu ya Mapinduzi ngoma za asili zinafanyika,” anasema Dk Omary akitolea mfano matamasha makubwa ya ZIFF na Sauti za Busara hivi sasa lipo na la Kizimkazi yanayofanyika visiwani humo.

“ZIFF na Sauti za Busara ni ya kimataifa zaidi, lakini kuna tamasha letu la asili lina miaka 28 lilianzishwa na Dk Salmin Amuor Juma (Rais mstaafu wa Zanzibar) hili linaakisi utamaduni halisi wa Mzanzibar.”

Anasema ngoma myingine ni ya Mwakakogwa ambayo ni ya jadi inafanyika Makunduchi, akifafanua kwamba ni mahususi kwa ajili ya kukoga mwaka ambako katika Uislamu kuna mwezi wa mfungo nne, wakitoka mwaka wa zamani kwenda mpya ndipo uchezwa ngoma hiyo

“Nyingine ni ngoma ya Pugwa ya huko Bumbwini ambayo inatumika kwa ajili ya mashetani, ambayo wagonjwa hupigiwa na kupona.

“Visiwa vya Pemba vina ngoma nyingi hasa kwenye maeneo ya Msuka, Mkoani na Mchangamdogo zaidi ya ngoma 300 na zina sababu, zipo za mavuno, sherehe, furaha na nyinginezo, mfano kwa Kizimkazi wana utaratibu kila mwaka baada ya funga sita wao ndiyo husherehekea.

“Donge kuna Ngoma ya Ndanda wanacheza wazee kuruka ruka na kupeana chambi, wale wazee wana afya sababu wana mazoezi na mtu yoyote wa Donge hata awe na cheo gani akiona ngoma hiyo atacheza, kuna ngoma ya kibati pia asili yake ni Pemba inatumika katika mavuno inakuwa na malenga anayetunga na kuimba papo kwa papo na waimbaji wa hii ngoma asilimia 95 ni wa ukoo wa Boha.

Dk Omary anasema Zanzibar vyakula vinavyopikwa ni vile vile ambavyo vinapatikana maeneo mengi, tofauti yake ni mapishi.

Akitaja baadhi ya vyakula maarufu visiwani humo, anasema ni mkate wa kiambazani ambao asili yake ni Uajemi, unaopikiwa kwenye tanuru.

“Huu ni mkate wa kuchoma, ambao unatengenezwa kwa ngano, hata pilau, linalopikwa Zanzibar ni tofauti na la Bara au India hata muhogo, mashelisheli, makopa, msambwija au ugali, ni vyakula vinavyopikwa maeneo tofauti, lakini mapishi ya Kizanzibar ni ya kitofauti kidogo hata kwenye biriani.”

Chanzo: Mwanaspoti