Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mfumo huu kuibeba Simba

39531 Pic+simba Mfumo huu kuibeba Simba

Mon, 4 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mifumo mitatu tofauti pamoja na matumizi ya mbinu tofauti za kujilinda, inaweza kuipa Simba ushindi ama sare kwenye mchezo wake dhidi ya Al Ahly huko Alexandria, Misri, Jumamosi hii.

Wawakilishi hao wa Tanzania kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, wanalazimika kuwa na uimara na ufanisi wa hali ya juu hasa katika safu ya kiungo na ulinzi ili kuhimili vishindo vya Al Ahly.

Idara za kiungo na ulinzi za Simba ndizo zinaweza kutoa muelekeo wa matokeo ambayo wawakilishi hao wa Tanzania wanaweza kupata mbele ya miamba hiyo ya Misri.

Katika siku za hivi karibuni, viungo na walinzi wa Simba wamekuwa wakifanya makosa ya mara kwa mara jambo ambalo limekuwa likiipa wakati mgumu Simba katika mechi ambazo imekuwa ikicheza.

Miongoni mwa michezo ambayo viungo na walinzi wa Simba walifanya makosa ni ule wa ugenini dhidi ya AS Vita katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo ilichapwa mabao 5-0 ugenini.

Kwa kutazama ubora wa kikosi cha Al Ahly, Simba inapaswa kuingia na mfumo bora ambao utawaweka kwenye mazingira ya kutopokea kichapo.

Badala ya mfumo wa 4-4-2 ambao kocha Patrick Aussems anapendelea kutumia, pengine mfumo 3-5-2 unaweza kumsaidia katika mchezo huo dhidi ya Al Ahly.

Aina hiyo ya mfumo inaweza kuwafanya Simba wawadhibiti Al Ahly upande wa pembeni ambako imekuwa ikitumia kutengeneza mabao.

Aina hiyo ya mfumo ilitumiwa na Simba mwaka jana ugenini dhidi ya Al Masry ya Misri ambapo zilitoka suluhu kabla ya Simba kuondolewa kwa sheria ya bao la ugenini baada ya mchezo wa nyumbani kumalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Mfumo mwingine 5-4-1, unaokuwa na mabeki watano ambao miongoni mwao, watatu wanasimama katikati huku mmoja akipewa jukumu la kufuta makosa ya wenzake.

Aidha, kwa kuwa Aussems ni muumini wa soka la kushambulia, anaweza kutumia mfumo 4-2-3-1 ambao utamfanya apange viungo wawili wa ulinzi watakaokuwa na jukumu la kuhakikisha ukuta wa Simba unakuwa salama lakini bado atakuwa na nguvu ya kushambulia akibebwa na viungo watatu watakaocheza nyuma ya mshambuliaji mmoja.

Kauli za makocha

“Ile ni mechi ngumu ngumu kwa Simba, lakini wachezaji wenyewe kama wataamua kufia uwanjani, watawaduwaza Waarabu.

“Wasiwasi wangu ni mabeki, washambuliaji sina presha nao, wana uwezo wa kufunga muda wowote, lakini kama mabeki wakimudu kulinda goli lao muda wote, wanaweza kushinda,” alisema Abdallah Kibadeni.

Kocha Ally Bushiri wa Mbao alisema Simba inapaswa kucheza kwa miiko inapokuwa ugenini.

“Wazingatie nidhamu ya mchezo, wafuate maelekezo na mbinu za kocha, lakini pia wachezaji wajiongeze, wajitambue na watambue majukumu ya kila mmoja uwanjani,”alisema Bushiri.

Kocha Mohammed Rishard ‘Adolf’ alisema nidhamu jambo la msingi kwa kuwa timu zote zina uwezo mzuri.

“Mbinu za kocha ndizo zitaipa Simba matokeo kule, cha msingi ni wachezaji kutulia na kudhibiti mashambulizi yote,” alisema Rishard.



Chanzo: mwananchi.co.tz