Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mengine haya hapa ushindi wa Simba!

33525 Pic+simba Tanzania Web Photo

Wed, 26 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Hakuna kilichotikisa medani ya soka nchini kama ushindi wa Simba wa mabao 3-1 dhidi ya Nkana Red Devils ya Zambia, katika mchezo wa kuwania kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika mchezo wa kwanza, Simba ililala 2-1 hivyo kutakiwa kushinda 1-0 nyumbani, lakini Walter Bwalya aliwatibulia alipoipa Nkana bao la kuongoza dakika ya 17 lililounyamazisha umati uliofurika kwenye Uwanja wa Taifa.

Kiungo Jonas Mkude alirudisha matumaini aliposawazisha dakika ya 29 kabla ya Meddie Kagere kuamsha nderemo alipofunga dakika za nyongeza kipindi cha kwanza na Clatous Chama akafanya yake dakika ya 88 akipiga bao lililoivusha Simba.

Nyuma ya matokeo

Kama ilivyoelezwa kuwa wachezaji watafia uwanjani, hakukuwa na mzaha hata kidogo, kwamba kila mmoja alijipanga kuhakikisha anatekeleza wajibu wake.

Hata wachezaji wenyewe hawakutaka kuona mmoja wao anapoteza muda uwanjani, hilo lilithibitika kwa kipa wa Simba Aishi Manula na beki Paschal Wawa ambao walipandishiana uwanjani damu zilipochemka.

Tukio la kupandishiana kwa Manula na Wawa lilimalizwa na Erasto Nyoni aliyewatuliza.

Kama ilivyo kawaida ya Manula akikamata mpira huzungumza, kitendo hicho kilionekana kumuudhi Wawa aliyemtaka apige mpira ndipo azungumze kwani muda ulikuwa unapotea na wakati huo Simba ilishafungwa bao 1-0.

Wakati wanapandishiana, Nyoni akaingilia kati na kusuluhisha ingawa haukuwa ugomvi bali ilitokana na damu kuchemka kama alivyoeleza baadaye Nyoni.

“Si kwamba ni ugomvi hasa au watu kutaka kupigana, ni maelekezo ya msisitizo kwa sisi wenyewe, kila mmoja analenga makubwa na anayezembea anaambiwa hata kwa ukali kuonyesha kuwa kila mmoja anapaswa kuwa makini uwanjani na damu ikichemka sio rahisi kuelekezana kwa kubembelezana,” alisema Nyoni.

Awali, bao la kutangulia la Simba liliwaibua Wawa na Manula kutokana na Wawa kujisahau na mara tu baada ya kupigiwa krosi, mfungaji alijiweka kwenye eneo la wazi na kuunganisha mpira kwa kichwa.

Hilo lilimfanya Manula kunyong’onyea kwa sekunde kadhaa kabla ya kuanza kuwabwatukia mabeki wake huku akiwa na mpira ndipo Wawa naye alipoanza kumlaumu kipa huyo kwa kuganda na mpira.

Wawa alichukia kuona Manula anapoteza muda kwa kuchelewa kupeleka mpira kati ili wapambane kusawazisha makosa yao, eneo la ulinzi la Simba lilionekana kuwa makini baada ya kufanya kosa hilo lililowagharimu.

Kiungo James Kotei naye alionekana kutupiana maneno na aliyekuwa beki wa kulia, Nicholas Gyan kabla ya kuumia na kutolewa, kuna wakati beki huyo alikuwa akipoteza mipira kirahisi kiasi cha Kotei kumtolea uvivu.

Matukio hayo yaliifanya Simba kutulia na kucheza kwa umakini na mwishowe wakapata mabao kupitia kwa Mkude na Kagere kipindi cha kwanza kabla ya Chama ‘Triple C’ kumaliza kazi kwa bao lake la kisigizo linalobaki kuwa gumzo.

Kuonyesha kuwa walikuwa hawataki kung’oka wachezaji wa Simba walijituma hadi Kagere na Gyan kuumia na kulazimika kupumzishwa na nafasi zao kuchukuliwa na Juuko Murshid na Hassan Dilunga aliyetengeneza bao la ushindi.

Hata baada ya kutoka Kagere aliendelea kuwahamasisha wachezaji wenzake walio uwanjani kupambana zaidi akishindwa kutulia kwenye benchi kadiri muda ulivyosonga, kila mara alisimama kama mmoja wa makocha wasaidizi ili kuwahamasisha wenzake.

Baada ya Chama kufunga, Kagere licha ya kuwa na maumivu alimkimbilia Mzambia huyo na kuanza kushangilia kwa staili yao tofauti ya kukutanisha mikono yao kwa kugongeana kiaina.

Simba ilianza safari ya kuwania tiketi ya kuingia makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwenye raundi ya awali kwa kucheza na Mbabane Swallows ya eSwatini.

Katika raundi hiyo, Simba ilisonga mbele kwa ushindi wa jumla ya mabao 8-1, walishinda mabao 4-1 nyumbani kisha kushinda 4-0 ugenini.

Hii ni mara ya pili kwa Simba kuingia hatua ya makundi ya michuano hiyo mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2003 ilipotinga hatua hiyo kwa mikwaju ya penalti 3-2 wakiivua ubingwa wa michuano hiyo Zamalek ya Misri.

Simba ambayo leo inacheza na Mashujaa ya Kigoma mchezo wa Kombe la Shirikisho FA, inasubiri droo ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa itakayopangwa keshokutwa jijini Cairo Misri .

Shirikisho la soka Afrika (CAF) limepanga pot nne zenye timu nne na kila pot itatoa timu moja kwenye kundi moja. Pot hizo zimepangwa kulingana na viwango vya ubora kwa klabu ndani ya miaka mitano iliyopita.

Pot 1 ina klabu za TP Mazembe (DR Congo) yenye pointi 66, Al Ahly (Misri-62), Wydad Casablanca (Morocco-51) na Esperance de Tunis ya Tunisia yenye pointi 45.

Pot 2 inaundwa na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini yenye pointi 40, AS Vita Club (DR Congo-29), Horoya (Guinea-19) na Club African (Tunisia) yenye pointi 12.

Pot 3 ina klabu za ASEC Mimosas ya Ivory Coast yenye point 8.5, Orlando Pirates (Afrika Kusini-8) FC Constantine (Algeria) na FC Platinum ya Zimbabwe ambazo hazina pointi.

Pot 4 inaundwa na Simba SC (Tanzania), Lobi Stars (Nigeria), Ismaily (Misri), JS Saoura (Algeria) zote hazina pointi. Kila pot itatoa timu moja kwa kila kundi, timu ambazo zipo pot moja haziwezi kupangwa kundi moja.



Chanzo: mwananchi.co.tz