Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mechi ya kwanza tu, Boban amefanya mambo

33519 Pic+boban Tanzania Web Photo

Wed, 26 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Juzi Jumatatu mashabiki wa Yanga walikuwa na shauku ya kumshuhudia kwa mara ya kwanza kiungo wao mpya, Haruna Moshi ‘Boban’ aliyecheza kwa dakika 26 kabla ya kuomba kutoka, kitendo kilichoibua mijadala kwa wadau wa soka.

Boban alisajiliwa hivi karibuni kwenye dirisha dogo akitokea African Lyon, usajili ambao ulikuwa gumzo licha ya kocha mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera kusisitiza kiungo huyo ana kipaji cha ajabu na uwezo wa kuisaidia Yanga.

Jumatatu Boban alicheza katika mchezo wa Kombe la Shirikisho (FA) dhidi ya Tukuyu Stars ya Mbeya na Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 4-0.

Boban aliyeshangiliwa na mashabiki wa Yanga kabla ya mechi kuanza, alithibitisha jicho la Mwinyi halikukosea kwani aliwatengea pasi za mwisho, Ibrahim Ajibu na Amiss Tambwe lakini hawakuzitendea haki pasi hizo.

Kabla ya mechi kuanza, Boban alionekana akimuelekeza kitu mshambuliaji wa Yanga, Heritier Makambo, dakika ya sita ya mchezo alitoa pasi ya mwisho kwa Ajibu ambaye alipiga shuti lililookolewa na kipa wa Tukuyu, New Afrika.

Dakika ya 25, kiungo huyo alimtengea pasi safi Tambwe ambaye pia hakuitendea haki kabla ya kuumia na kuomba kutoka dakika ya 26 na nafasi yake kuchukuliwa na Deus Kaseke.

Hata hivyo kwa dakika 26 alizocheza kiungo huyo zimewaibua wachambuzi wa soka nchini, Ally Mayay na Alex Kashasha ‘Mwalimu Kashasha’ ambao wamezungumzia uwezo wa Boban na aina ya timu anayoichezea sasa.

“Binafsi naona Boban alicheza vizuri tena katika mechi yake ya kwanza jana (juzi), alitoka baada ya kuumia, lakini hilo haliwezi kuwa tatizo kubwa sababu hana historia ya kuwa majeruhi.

Bado ana uwezo wa kumiliki mipira na kutoa pasi zaidi ya Ajibu niseme kuwa bado sijamuona kiungo wa kiwango cha kumshinda Boban pale Yanga, licha ya umri wake kusogea lakini ana kipaji cha soka,” alisema Mayay.

Mwalimu Kashasha alisema kwa kiwango cha Boban kwa sasa sio mchezaji wa kuhimili kucheza dakika 90, lakini katika mechi ya juzi alicheza vizuri kwa muda wote kabla ya kuumia.

“Hayuko fiti kumudu kucheza dakika 90, sababu hayuko katika hali ya ushindani kiakili, aandaliwe ili awe tayari kucheza mechi za upambanaji, ingawa jana (juzi) kipaji chake kilimbeba,” alisema Kashasha.



Chanzo: mwananchi.co.tz