Mechi ya Ligi Kuu Bara yamfanya mmiliki shule za Alliance kushindwa kuzungumzia matokeo darasa la saba yaliyofutwa
Mwanza. James Bwire, mmiliki wa shule za New Alliance na Alliance zilizofutiwa matokeo yake ya mtihani wa Taifa wa darasa la saba kutokana na kufanya udanganyifu na kuvujisha mtihani, ameshindwa kuzungumzia uamuzi huo wa Baraza la Mitihani (Necta) kwa kuwa alikuwa akitazama mechi ya Ligi Kuu Bara.
Mechi hiyo imechezwa leo jioni Oktoba 2, 2018 katika uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza kati ya timu anayoimiliki ya Alliance FC dhidi ya Ndanda FC. Bwire pia anamiliki timu ya Alliance Girls FC na Nyamwaga FC.
Alipoulizwa na MCL Digital kuhusu uamuzi huo wa Necta uliotangazwa leo mchana, Bwire amesema hawezi kuzungumza kwa sababu alikuwa na majukumu mengine ikiwa ni pamoja na kutazama timu yake ikicheza uwanjani.
“Usinilazimishe kuzungumza kwa sasa kuna mambo ninayashughulikia. Tutawasiliana jioni nipo uwanjani natazama mpira,” amesema Bwire ambaye pia ni Meya wa Jiji la Mwanza.
Mbali na shule za Alliance, nyingine zilizokumbana na rungu hilo ni shule zote za msingi za Halmashauri ya Chemba mkoani Dodoma, shule Kondoa Integrity iliyopo mji wa Kondoa mkoani Dodoma; Hazina, New Hazina, Aniny Nndumi na Fountain Of Joy (Dar es Salaam) na Kisiwani ya Mwanza.
Necta imeeleza namna shule hizo zilizofanya udanganyifu wa kuvujisha mtihani ya Taifa ya darasa la saba iliyofanyika Septemba 5 na 6, 2018.
Necta imesema katika shule hizo mitihani ya Taifa ya darasa la saba itarudiwa Jumatatu na Jumanne ijayo katika vituo vitakavyopangwa. Mechi kati ya Alliance FC na Ndanda imemalizika 0-0.