Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mechi moja ya Taifa Stars inavyogonganisha watu vichwa

64532 STARS+PIC

Thu, 27 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mjadala unaoendelea kila kona nchini ni ushiriki wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ katika michuano ya mataifa Afrika (Afcon) inayofanyika nchini Misri ikishirikisha nchi 24 kutoka barani humo.

Tayari Stars imeshajitupa uwanjani kucheza mchezo wake wa kwanza dhidi ya Senegal na kulala kwa mabao 2-0 mbele ya vigogo hao wanaokamata namba moja kwa ubora wa soka Afrika.

Tangu kufungwa na wababe hao maarufu Simba wa Teranga ambao ndani ya kikosi chao hakuna mchezaji yeyote anayecheza katika ligi za Afrika huku wengi wakiwa wanacheza ligi kuu tano zenye ubora zaidi barani Ulaya ikimaanisha England, Hispania, Ufaransa, Italia na Ujerumani, mambo mengi yamejadiliwa na wengi wameibuka.

Kila mmoja anasema lake wapo watalaamu wa soka na michezo, wachambuzi na hata wanasiasa nao wameingilia kati lakini kubwa zaidi ni mhimili wa Bunge na Serikali nayo ikijitosa huku misuli ikitunishwa.

Wabunge na mawazo kutoka Misri

Katika kuunga mkono na kuongeza hamasa, kundi la wabunge 50 wakiongozwa na Spika Job Ndugai walikwenda Cairo, Misri kuongoza hamasa katika ushangiliaji wakati wa mchezo huo wa kwanza ulioshuhudia mchezaji Keprin Diatta anayekipiga katika klabu ya Club Blugge ya Ubelgiji akipata umaarufu mkubwa Tanzania, picha yake imesambazwa kwa namna tofauti kwenye mitandao ya kijamii, ni baada ya kufunga goli la pili lililozima kabisa ndoto za Watanzania kuandika historia mbele ya vigogo hao kwa ushindi au japo kupata sare.

Pia Soma

Ndiatta kufunga goli sio tatizo ila shuti lake kali lililomfanya golikipa wa Stars Aishi Manula (Tanzania One) aishie kuusindikiza kwa macho hadi wavuni, ndilo lililoonekana kuwagusa wengi.

Wabunge wakiwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), wakirejea baada ya mchezo huo wakatoa maoni yao kuhusiana na kile walichokishuhudia Misri hasa katika kambi ya Taifa Stars.

Walieleza mengi lakini mojawapo ni kutaka kuendelea kuungwa mkono kwa timu hiyo ili ifanye vyema. Spika Ndugai, alisema kuna kila sababu ya kuendelea ‘kuwasapoti’ wachezaji wa Stars kwani wamecheza na timu ambayo inashika namba moja kwenye viwango vya soka Afrika.

“Senegal ina wachezaji wengi wazuri ambao wanacheza nje, hivyo kwa matokeo yale, inatubidi tuendelee kuwasapoti wachezaji wetu kwani hata baada ya mechi kwisha, walituahidi watafanya vizuri kwa mechi zilizobaki,” alisema. Kwa mujibu wa Ndugai, michuano hiyo imetoa funzo kuwapo kwa haja ya kuwekeza katika michezo, hasa soka, kutoa mafunzo kwa makocha, waamuzi na kuondoa rushwa kwenye sekta hiyo.

Kwa upande wake mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko, alisema kuna haja ya kuanzishwa kwa kituo cha soka la vijana (academy). “Ni vizuri mpira wa miguu ukaanzia kwenye shule za msingi, sekondari, wachezaji wakapatiwa vifaa vya michezo, hii itatusaidia kufanya vizuri baadaye,” alisema.

Naye Mbunge wa Kuteuliwa, Abdallah Bulembo, alilinyooshea kidole Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Kocha Mkuu wa Stars Emmanuel Amunike kutokana na kile alichodai upangaji mbovu wa kikosi kilichoivaa Senegal.

“Timu iliyopangwa, sehemu ya viungo ilionekana kuzidiwa, kocha alitakiwa kuangalia mapema ni wapi tulizidiwa ili aweze kufanya marekebisho mapema,” alisema.

Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia, alihoji: “Kocha wa timu ya Taifa ana rekodi gani hadi apewe timu? Nilikaa na Rais wa Chama cha Soka cha Nigeria, alisema kama angepata nafasi ya kutupa ushauri, angetuambia yule sio kocha, lakini pamoja na yote, Tanzania tunatakiwa tuwekeze kwenye timu ya Taifa.”

Mbunge wa Urambo, Magreth Sitta, alisema vijana wapo vitani, lugha ambayo inatakiwa itumike ni kuwapa moyo.

Msikie Makonda sasa

Katika hafla ya uzinduzi wa kiwanda cha gesi cha Taifa, Kigamboni juzi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda naye akatoa maoni yake kwa timu hiyo huku akionyesha kusikitishwa na kauli za baadhi ya wabunge kwa Stars.

“Mimi ni mpenzi mkubwa wa Taifa Stars na nimeumizwa sana na matokeo ya Senegal, lakini kilichoniuma kikubwa zaidi ni watu kuwabeza wachezaji wa Taifa Stars ambao wameipa heshima nchi hii kwa miaka 39 kuingia Afcon 2019, leo wameonekana hawana afya njema, hawana chochote, hawana uongozi mzuri, hatuwezi kuwa na taifa la namna hii.

“Mheshimiwa Rais, kama itakupendeza ninaomba unipe ruhusa niende Misri kuwapa hamasa vijana wetu, nina uhakika watashinda mechi ijayo dhidi ya ndugu zetu Kenya. Vijana wetu wana ari kubwa ya ushindi, hata leo (juzi) asubuhi nimeongea na nahodha Mbwana Samatta, amenihakikishia wapo vizuri na watashinda mechi ijayo,” alisema.

Hata hivyo, Spika Ndugai akijibu mwongozo wa Mbunge wa Kigoma mjini Zitto Kabwe, aliyehoji kauli ya kiongozi mmoja wa Serikali aliyodai inadhalilisha Bunge.

Ndugai alisema, “hayo ni mawazo ya mtu ambaye kidogo ndio hivyo. Ni bahati mbaya sana tuna viongozi wa Serikali wanadiriki kumdanganya Rais hadharani, kiongozi wa Serikali unapoongea mbele ya rais jipange ongea ukweli mtupu wa mwenyezi mungu usisingizie wala kumuone mtu hatufanyi hivyo”.

JPM apongeza

Rais John Magufuli akitoa neno kwa Taifa Stars kuhusiana na michuano hiyo baada ya kuombwa na Makonda katika hafla hiyo, aliwatia ujasiri wachezaji akiwataka kupambana katika mechi mbili zilizobaki dhidi ya Kenya inayopigwa leo na ile ya Julai 1, dhidi ya Algeria.

Aliwaka wachezaji kutokatishwa tamaa na baadhi ya watu wanaowaponda baada ya kupoteza katika mchezo wa kwanza wa Kundi C.

Rais alisema kufungwa na Senegal haina maana Taifa Stars ni timu dhaifu, hivyo amewataka kujiandaa vyema kwa mechi mbili zilizobaki za hatua ya makundi “Mwanzo si mbaya kufungwa na timu inayoongoza Afrika tena mabao 2-0 huku wachezaji wa wenzetu wote wanacheza nje. Wachezaji wapewe moyo kwa sababu wakifungwa tunafungwa Tanzania na wakishinda basi inashinda Tanzania, kwenye uwanja wa mpira kuna kushinda na kushindwa sisi tutaendelea kuwaombea,” alisema Rais Magufuli.

Aidha, alimpa ruhusa Makonda kwenda Misri kuongeza morali kwa wachezaji, akisema ana matumaini Taifa Stars itafanya vyema dhidi ya Kenya.

Hali halisi

Kinachotokea sasa ni kama kunyoosheana vidole wakati kila mmoja akipaswa kutimiza wajibu wake katika hatua mahususi, wabunge wanapojadili mafanikio ya soka wanapaswa kulitazama jambo hilo kwa upana, kutoa mawazo ya kujenga na kutenga fedha za kutosha kwa maendeleo ya soka na sio kiduchu ambazo matokeo yake ni kushindwa kupiga hatua.

Mdau wa soka na mwekezaji mwekezaji wa klabu ya Simba, Mohamed Dewji aliandika katika mtandao wake wa Tweeter akitaka Taifa Stars ipewe nafasi na isihukumiwe kwa matokeo ya mchezo wake na Senegal.

“Ni rahisi kuchambua mapungufu ya TaifaStars uwanjani lakini naomba tusilalamike sana. Hebu tutazame kikosi cha Senegal kisha tukitathmini na chetu. Wachezaji wao wapo Barcelona, Liverpool, Everton. Ukiacha uwezo (skill) wenyewe, uzoefu (experience) na ‘exposure’ ni kila kitu!” aliandika Mo Dewji.

Kocha Amunike anasema yaliyopita yamepita na sasa ameiandaa timu hiyo kushindana na Kenya na mechi hiyo itakuwa ya kufa au kupona ana imani na kikosi chake, amewapa wachezaji ushauri wa kisaikolojia kabla ya kuvaana na Kenya akiamini watafanya vizuri.

Chanzo: mwananchi.co.tz