Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mdomo wamponza kocha Zahera

74353 Zahera+pic

Thu, 5 Sep 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kamati ya Bodi ya Ligi Kuu ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imemfungia mechi tatu kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera kwa kutoa shutuma na kejeli kwa Bodi ya Ligi huku pia ikimfungia miezi mitatu mwamuzi wa pembeni Janeth Balama.

Kamati hiyo imedai Zahera aliishutumu Bodi ya Ligi katika mkutano na waandishi wa habari baada ya mechi kati ya Yanga dhidi ya Ruvu Shooting hivyo adhabu hiyo imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 41(9) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Makocha.

Pia kamati hiyo imempiga faini ya Sh 500,000 kocha huyo raia wa DR Congo kwa kuvaa mavazi yasiyo nadhifu na ya heshima katika mechi hiyo kinyume cha Kanuni ya 14(2m) ya Ligi Kuu kuhusu taratibu za mchezo.

Kikao cha kamati hiyo kilichofanyika juzi na kupitia matukio mbalimbali ya Ligi Kuu msimu wa 2019/2020 pia kimeipa Yanga onyo kali kwa kushindwa kuhakikisha Kocha wake Zahera anaongoza benchi la ufundi la timu yake akiwa katika mavazi nadhifu na ya heshima na adhabu dhidi ya klabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 14(3) ya Ligi Kuu kuhusu taratibu za mchezo.

Pia mwamuzi msaidizi katika mchezo kati ya Yanga na Ruvu Shooting, Janeth Balama amefungiwa miezi mitatu kwa kushindwa kutafsiri sheria, hivyo kusababisha akatae bao halali lililofungwa na Ruvu Shooting katika mechi hiyo iliyofanyika Agosti 28 ambayo ilimalizika kwa Ruvu Shooting kushinda bao 1-0.

Kamati hiyo haijamuacha salama Msemaji wa Ruvu Shooting, Masau Bwire, ikimpiga faini ya Sh 200,000 kwa kosa la kuingia ndani ya uwanja (eneo la kuchezea) baada ya filimbi ya mwisho kinyume cha Kanuni ya 14(10) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo. Adhabu dhidi yake imetolewa kwa kuzingatia Kanuni ya 14(49) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Pia Soma

Advertisement
Katika hatua nyingine, klabu ya Yanga imekanusha kumpa kocha wake Zahera mechi tatu akishindwa afukuzwe.

Msemaji wa Yanga ambaye pia ni Kaimu Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Dismas Ten amesema uongozi hawaujawahi kufikiria kumtimua kocha huyo.

Chanzo: mwananchi.co.tz