Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbunge ashauri ongezeko kodi wachezaji wa kigeni

56214 Pic+wachezaji

Wed, 8 May 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati wanasoka wa kigeni wanaocheza ligi mbalimbali duniani wakibanwa na makato ya kodi kwenye mishahara na fedha wanazoingiza, hali imekuwa tofauti kwa wanaoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.

Wachezaji wa kigeni wanaocheza timu tofauti za Ligi Kuu na Daraja la Kwanza wanakatwa kiwango sawa cha asilimia ya kodi kwenye mishahara sawa na kile kinachokatwa kwa wachezaji wazawa.

Mkurugenzi wa Elimu na Huduma kwa Walipa Kodi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Richard Kayombo aliliambia Mwananchi mamlaka hiyo imekuwa ikikata kiwango sawa cha asilimia katika mishahara ya wanasoka nchini pasipo kuangalia uraia wa mchezaji husika kama ambavyo baadhi ya nchi zinafanya.

“Wachezaji ni wafanyakazi kama ilivyo kwa wengine na kodi wanayokatwa kwenye mishahara yao ni asilimia ileile, hivyo inategemeana na kiwango cha mshahara ambacho mtu anakatwa,” alisema Kayombo.

Hata hivyo wakati nyota wa kigeni wakikatwa kiwango sawa cha asilimia ya kodi katika mishahara kama wanachokatwa wazawa, hali iko tofauti katika nchi mbalimbali ambako nyota wa kigeni hukutana na kodi kubwa na wazawa wakipata mteremko.

Baadhi ya nchi hizo zimeweka kiwango kikubwa cha makato katika mishahara ya wageni ili fedha hizo zirudi kusaidia shughuli na huduma za kijamii, kutokana na uhalisia kuwa wachezaji wengi wa kigeni wamekuwa wakienda kuwekeza fedha hizo katika nchi zao badala ya nchi wanakocheza.

Katika Ligi Kuu England, mchezaji wa kigeni hukatwa asilimia 45 ya kodi katika mshahara wake wakati Hispania, fedha ya kodi anayokatwa mchezaji wa kigeni ni asilimia 52.

Wakati mchezaji wa kigeni anayecheza Ligi Kuu Ujerumani akikatwa asilimia 47.475 ya kodi kwenye mshahara wake, Italia anakatwa asilimia 46.29 kwenye mshahara anaolipwa. Kwa upande wa Tanzania yenye idadi ya wachezaji wa kigeni zaidi ya 40, mchezaji anakatwa asilimia 30.

Akizungumza jana, Mbunge wa Mafinga Mjini, Cosato Chumi alisema ipo sababu ya kuweka mkazo wa kodi kwa wachezaji wa kigeni.

“Hili ni jambo ambalo lipo hata kwenye mpango wangu wa Bunge. Unajua kama mgeni anakuja kama mwekezaji si vibaya kumpunguzia kodi kwasababu atawekeza na atasaidia kupatikana ajira.

“Lakini hapa tunazungumzia wachezaji ambao naamini kama akina Emmanuel Okwi na Amissi Tambwe zaidi ya asilimia 80 ya mshahara wao wanakwenda kuwekeza kwao, hivyo nchi inapaswa kunufaika kutokana na uwepo wao. Hatusemi kama hatutaki waje ila ni lazima tutengeneze mazingira ambayo yatasaidia nchi kunufaika,” alisema Chumi.

Katibu mkuu wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah alisema ingawa ni utaratibu wa kisheria kwa wachezaji kukatwa kodi, wachezaji wa kigeni wanapaswa kuchangia zaidi pato la nchi.

“Wachezaji wengi wa kigeni wanalipwa mishahara mikubwa hivyo hata wakikatwa hizo asilimia za kodi, bado wanabaki na kiasi kikubwa cha fedha mkononi ambacho kama kingekatwa kingeisaidia kutumika kwenye shughuli nyingine za kijamii.

Lakini hata hivyo ifahamike hata Ulaya, sheria hiyo haiwahusu wachezaji tu bali hata wafanyakazi wengine hivyo hata ikibadilishwa haitawagusa wachezaji tu,” alisema Osiah.



Chanzo: mwananchi.co.tz