Zaidi ya watu 1,000 wanatarajia kushiriki mbio za ‘Figo Marathon’ zitakazofanyika Julai 9, 2023 katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam kwa lengo la kuwezesha kukusanya fedha kwaajili ya wagonjwa wa figo.
Mbio hizo zinazoandaliwa na Taasisi ya Healthier Kidney Foundation (KHF), kwa kushirikiana na Hospitali ya Taifa Muhimbii (MNH) zinafanyika kwa mara ya pili na mwaka huu lengo likiwa ni kutoa elimu na kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu magonjwa ya figo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Ijumaa Juni 30, 2023, Mkurugenzi Mtendaji wa MNH Profesa Mohammed Janabi amesema mgeni rasmi katika mbo hizo anatarajiwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila.
“Niwashukuru waandaaji wa Figo Marathon, hii siyo mara yao ya kwanza ila nafikiri kwa mwaka huu imekuwa kubwa zaidi,” Profesa Janabi amesema huku akitoa rai kwa watu kujitokeza kuwachangia wenye shida ya figo hapa chini.
Fedha zitakazopatikana katika mbio hizo zitawasaidia wagonjwa wanaofanya huduma ya kuchuja na kusafisha damu hospitalini hapo.
Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa HKF Jenipher Mambo amesema gharama ya kushiriki Figo Marathoni ni Sh35, 000 kwa mtu mmoja na anaweza kushiriki yeyote hata watoto.
Amesema mbio zitaanzia na kumalizikia viwanja vya Mnazi Mmoja na zitaanza saa 12 asubuhi ambapo kutakuwa na mbio za kilometa tano, 10 na 21.