Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbili za kupanda FDL kujulikana leo

Fdl Pic Data Mbili za kupanda FDL kujulikana leo

Mon, 17 May 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Mwanza. Hatma ya timu mbili za kupanda Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao itafahamika leo Jumatatu pale timu za Tunduru Korosho, Green Warriors, Mashujaa na DTB zitakaposhuka uwanjani katika mechi zao za mwisho.

Timu hizo ambazo zimegawanywa makundi mawili, kila upande utatoa timu moja kinara ambayo itapanda moja kwa moja daraja la kwanza msimu ujao huku nyingine zikisalia kwenye ligi daraja la pili.

Katika mechi hizo, Tunduru Korosho itawakabili vinara Green Warriors katika mchezo wa kundi A, ambapo timu hiyo inahitaji ushindi wa kuanzia mabao mawili ili kujihakikishia kupanda daraja la kwanza.

Kwenye kundi hilo, Green Warriors wana pointi tatu sawa na Pan African licha ya kuwa mbele kwa bao moja, huku Tunduru Korosho wakiwa mkiani bila alama yoyote na kufanya mchezo huo kuwa mkali.

Green Warriors ambao waliwahi kuwatibulia Simba katika mchezo wa kombe la Shirikisho kwa kuwafunga mabao 4-3 kwa mikwaju ya penalti msimu wa 2017/18, watahitaji aidha sare au ushindi ili kupanda daraja.

Kwa upande wa kundi B, Mashujaa ambao mechi ya kwanza walitoa sare ya bao 1-1 dhidi ya Kurugenzi, watakuwa na kazi nzito kuwavaa vinara DTB wenye pointi tatu wakihitaji aidha sare au ushindi ili kwenda daraja la kwanza.

Kocha wa Tunduru Korosho, Kessy Mzirai amesema wanaingia dimbani kwa lengo moja tu, kusaka ushindi na idadi kubwa ya mabao ili kukwepana na wapinzani wao, Pan African.

"Leo ni kufa au kupona, tunahitaji ushindi wenye idadi kubwa ya mabao ili kujihakikishia kupanda daraja kama malengo yetu yalivyo, tumejiandaa na vijana wako fiti na tayari kwa mapambano" amesema Mzirai.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz