Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbeya City yapigwa kotekote, Biashara yaisoma namba, Kagera Sugar yabanwa

15179 Pic+mbeya+city TanzaniaWeb

Sun, 2 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Tanga/Mikoani. Mbeya City imeendelea kupigwa, baada ya jana kupoteza mchezo wake wa tatu mfululizo tangu kuanza ligi hiyo msimu huu.

Wakati Mbeya City ikifanya madudu, Biashara Mara imeendelea kuisoma namba baada ya jana kuonyeshwa Ligi Kuu inachezwaje kwa kuchapwa bao 1-0 na Stand United.

Mchezo wa Mbeya City kufungwa ni wa tatu kwani ilianza kufungwa mabao 2-0 na Azam kabla ya kupigwa idadi hiyo na Simba na jana ikalala kwa Mtibwa 2-1 na kuonyesha kuwa msimu huu huenda ikarudi Ligi Daraja la Kwanza kwa mwendo iliouanza.

Biashara iliyoanza Ligi kwa kishindo ikiishinda Singida United 1-0 ugenini kwenye Uwanja wa Namfua jana ilijikuta ikifungwa bao hilo moja na ‘Chama la Wana’ kwenye Uwanja wa CCM Kambarage mkoani Shinyanga.

Stand ilipata bao lake dakika ya 60, kupitia kwa Mrundi Bigirimana Blaise kwa shuti.

Kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga, mashabiki wa Coastal Union walishindwa kukata kiu ya kumuona mshambuliaji wao mpya, Ali Kiba akiitumikia timu hiyo wakati Coastal Union ikiialika KMC ya Dar es Salaam.

Hata hivyo, mchezo huo ulimalizika kwa sare ya bao 1-1. Alikiba msanii nyota wa bongo fleva, alionekana uwanjani ingawa alikaa jukwaani.

Shauku ya mashabiki wa timu hiyo ni kumuona dimbani kwani bado hajaichezea hata mchezo mmoja tangu asajiliwe kutokana na kuwa na majukumu ya kimuziki nje ya Tanzania.

Katika mkataba wake na Coastal kutokana na kuridhia kuitumikia timu hiyo bila malipo, mchezaji huyo anaruhusiwa kuondoka kambini na kwenda kufanya onyesho au kazi nyingine za kimuziki.

Hata hivyo, Alikiba aliliambia Mwananchi jana kuwa anatarajia kuanza kuitumikia rasmi katika mchezo ujao, kwani ameshamaliza ziara za kimuziki zilizompeleka Marekani na Canada.

Matokeo mengine, Tanzania Prisons imeichapa Alliance FC ya Mwanza mabao 2-0 huku Kagera Sugar ikishindwa kutamba katika uwanja wao wa nyumbani wa Kaitaba baada ya kutoka suluhu na African Lyon ya Dar es Salaam.

Chanzo: mwananchi.co.tz