Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbelgiji Simba akunjua makucha mapema

90148 Mzungu+pic Mbelgiji Simba akunjua makucha mapema

Sat, 28 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Licha ya kutoa dozi katika mechi mbili, kocha wa Simba Sven Vandenbroeck amesema haridhishwi na kiwango cha wachezaji wake.

Sven ametoa kauli hiyo alipozungumza na gazeti hili baada ya Simba kushinda mabao 4-0 dhidi ya Lipuli, Dar es Salaam. Pia aliiongoza timu hiyo kuifunga AFC Arusha mabao 6-0 katika mechi ya Kombe la FA.

Kocha huyo alisema mabao 10 aliyopata katika mechi mbili si kipimo cha ubora wa wachezaji wake na ameahidi kuchukua hatua kwa mchezaji mzembe.

Alisema alichobaini katika mechi hizo mbili, Simba imekuwa ikifanya makosa ya kizembe kadri muda wa mchezo unavyokwenda licha ya kuanza vyema.

Kocha huyo raia wa Ubelgiji aliyejaza nafasi ya Patrikc Aussems, alisema hana sababu ya kuongeza idadi ya wachezaji katika usajili wa dirisha dogo kwa kuwa waliopo ni bora, lakini hawajitumi.

Alisema malengo yake ni kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo hawezi kuwa na wachezaji wasiojituma ambao watakwenda kushindana na miamba ya soka kama TP Mazembe ya DR Congo au Al Ahly ya Misri.

“Timu haina uhitaji mkubwa wa kuongeza wachezaji katika dirisha dogo, maeneo mengi tumekamilika na kila mchezaji anayecheza nafasi hiyo ana uwezo wa kufanya kazi ipasavyo.

“Nimeanza kuwa mkali na kuwaeleza sijaridhika na kiwango wanachokionyesha katika mashindano ya ndani wataonekana imara, lakini tutashindwa kufikia malengo makubwa mwakani,”alisema Sven.

Katika kuthibitisha hilo, Sven anasema katika mchezo dhidi ya Lipuli Simba ilicheza kwa kiwango bora dakika 21 za mwanzo kabla ya kufanya makosa mengi kadri muda ulivyokuwa ukiendelea.

“Baada ya dakika 21 hatukucheza vizuri tulifanya makosa ambayo kama tungecheza na timu bora yenye wachezaji wazuri yangekuwa madhara kwetu,”aliongeza Sven.

Kocha huyo alisema ataendelea kupangua kikosi kutokana na ratiba kuonyesha watakuwa wakicheza mechi idadi kubwa ya mechi ndani ya wiki mbili. Katika mchezo dhidi ya Lipuli alimuanzisha kiungo Hassan Dilunga ambaye amekuwa akiingia akitokea benchi. Dilunga alifunga mabao mawili.

Chanzo: mwananchi.co.tz