Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbelgiji Simba aipigia hesabu kali Mbao

18425 Pic+mbao TanzaniaWeb

Fri, 21 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Kocha Patrick Aussems wa Simba amesema amewasoma wapinzani wao Mbao FC na mkakati wake ni kupata ushindi, baada ya kutoka suluhu katika mechi iliyopita dhidi ya Ndanda.

Akizungumza mjini hapa, Aussems alisema haitakuwa kazi rahisi kupata ushindi kwa kuwa Mbao ni timu ngumu na imeanza vyema mashindano hayo msimu huu.

Aussems alitoa kauli hiyo jana jioni, baada ya Simba kufanya mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wa CCM Kirumba utakaotumika kwa mechi hiyo.

Simba inacheza mchezo wa nne wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, baada ya kuvuna pointi saba katika mechi tatu za awali.

Mabingwa hao wa Ligi Kuu waliifunga Tanzania Prisons bao 1-0 kabla ya kuilaza Mbeya City mabao 2-0 na baadaye ilitoka suluhu na Ndanda, hivyo leo wanahitaji ushindi ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kutetea ubingwa msimu huu.

“Wachezaji wote wapo vizuri na malengo yetu ni kupata pointi tatu, Mbao ni timu nzuri imeanza vyema ligi kwa hiyo tutawakabili kwa tahadhari ili kutimiza azma yetu,” alisema Aussems.

Kocha huyo raia wa Ubelgiji, alisema amependa hali ya hewa, mazingira ya uwanja ni mazuri na alisisitiza kuwa atahakikisha wachezaji anawaweka vizuri kisaikolojia ili kupata pointi tatu ugenini.

“Kwa ujumla hali ya hewa ni nzuri na uwanja nimeukubali kikubwa ni kuwaandaa vyema wachezaji kisaikolojia ili nafasi watakazopata waweze kuzitumia vyema, matarajio yetu si sare wala kupoteza, tunataka ushindi,” alisisitiza kocha huyo.

Naye Kocha wa Mbao, Amri Said alisema anahitaji kuondoa uteja wa kufungwa na Simba.

“Tunawaheshimu wapinzani wetu Simba kutokana na uzoefu wao, lakini hatuwezi kukubali kupoteza mchezo wa pili mfululizo tena nyumbani, tumejipanga kutoa ushindani na lengo letu ni kushinda,” alisema Said aliyewahi kuwa beki kisiki wa Simba.

Kocha huyo wa zamani wa Lipuli, alisema hakuna mchezaji majeruhi na wachezaji wote wameandaliwa kisaikolojia kucheza kwa nguvu na ari ya kupata matokeo mazuri katika mchezo huo unaotarajiwa kuwa na msisimko mkali.

Chanzo: mwananchi.co.tz