Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbelgiji Simba aanika silaha za maangamizi

10784 PIC+SIMBA TanzaniaWeb

Wed, 8 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Leo ndio Leo siku ambayo mashabiki wa Simba na wapenzi wa soka walikuwa wakiisubiri kwa hamu kushuhudia silaha mpya za timu hiyo katika Tamasha la Simba Day imewadia.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Kocha wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussems alisema amewaona wachezaji wote wa Simba na amefurahishwa na viwango vyao.

Aussems alisema mipango yake ya kwanza ilikuwa kutafuta wachezaji 18 ambao watakuwa fiti kuliko wengine katika kila nafasi na atawapa kipaumbele cha kuwatumia katika mechi nyingi.

Alisema falsafa yake ni kucheza soka ya kushambulia haraka na wakipoteza mpira ni kukaba kuanzia mbele jambo ambalo mchezaji ambaye hatakuwa fiti asilimia 100 atashindwa kuwa chaguo lake la kwanza.

“Ukiangalia kikosi ni kipana kina wachezaji zaidi ya 30 na kila sehemu wapo zaidi ya wawili ambao wana uwezo wa kucheza, kwahiyo kazi yangu itakuwa kuangalia ambaye yupo fiti zaidi ya mwenzake.

“Upana wa kikosi kuwa na wachezaji wengi hainiumizi kichwa napenda ushindani kwa wachezaji na nimekuwa nikifanya hivyo katika timu zote nilizofundisha kwahiyo upana wa kikosi ndio nataka. “Timu ambayo nilikuwa nikipanga kule Uturuki hakuna kikosi cha kwanza nilikuwa nikiwajaribu na katika wachezaji wangu niliokuwa nao yeyote anaweza kuwa katika kikosi cha kwanza.

“Mchezaji yeyote ambaye atakuwa akifanya ninavyotaka na kumuagiza ndio ataingia katika wale 18 ambao watakuwa fiti na kuwatumia mara kwa mara, “ alisema Aussems.

“Washambuliaji, viungo, mabeki na makipa ambao wote nilikuwa nao nina nafasi ya kuwatumia lakini ambao watafanya au kufuata mimi ninavyotaka watakuwa wakicheza katika malengo na falsafa zangu.

“Nafahamu nina makipa watano lakini hawa watatu ambao nilikuwa nao katika kambi nchini Uturuki ndio nitawatumia msimu huu labda itokee sababu nyingine maalumu,” aliongezea Aussems.

Alisema nahodha wa Simba John Bocco atakosekana katika mechi ya leo dhidi ya Asante Kotoko kwasababu ya majeruhi ingawa atakuwa miongoni mwa nyota watakaotambulishwa.

“Bocco atakosekana katika mechi hii alipata majeraha nimeona vyema apumzike akapate matibabu zaidi na kupona haraka, “ alisema kocha huyo.

“Wachezaji wote wana nafasi ya kutumika katika mechi ya leo, nachukulia kama mechi ya kirafiki na si kujali matokeo kwa hiyo naomba mashabiki wa Simba wajitokeze kwa wingi kushuhudia timu yao,” alisema Aussems.

“Nimeiona Simba katika luninga ni timu kubwa Afrika na wanacheza vizuri, lakini tumejipanga kushindana nao na kupata ushindi katika mechi hii ndio maana tumekuja na kikosi chetu kamili, “ alisema kocha wa Asante Kotoko Fabian Samwel.

Asante Kotoko ni miongoni mwa klabu kubwa Ghana na imewahi kutamba katika soka ya Afrika.

Chanzo: mwananchi.co.tz