Michezo

Habari

Burudani

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbelgiji Simba SC awatega Waarabu

39330 Ausems+pic Mbelgiji Simba SC awatega Waarabu

Mon, 4 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kocha Patrick Aussems ametoa kauli ya mtego kwa Al Ahly, lakini kama amemaanisha, mashabiki wa Simba hawapaswi kuwa na matarajio ya timu hiyo kupata ushindi katika mechi yao itakayochezwa Jumamosi wiki hii mjini Alexandria, Misri.

Muda mfupi baada ya msafara wa Simba kuwasili Alexandria itakapochezwa mechi hiyo kwenye Uwanja wa Borg El Arab, Aussems alisema hadhani kama timu yake itapata angalau pointi moja katika mchezo huo, kauli ambayo inaweza kuwa ya kiufundi ili kuwahadaa wapinzani wao.

Akinukuliwa na kituo cha luninga cha Sada El-Balad, Aussems alisema Al Ahly ni timu bora Afrika na imeizidi Simba mambo mengi.

“Ni mechi muhimu mno.Tunajua tunakutana na timu imara Afrika kwa kipindi cha miaka 10 ya hivi karibuni. Mechi itakuwa ngumu na tunatakiwa kufanya kazi ya ziada.

“Niwe mkweli. Sikutarajia na sidhani kama tunaweza kupata pointi kutoka kwa AS Vita na Al Ahly kwenye mechi za ugenini. Mkazo wetu ni kukusanya pointi nyumbani. Huwa sipendelei ndoto hatuwezi kupata pointi kwasababu watapata penalti, mchezaji wetu mmoja ataonyeshwa kadi nyekundu na pia watapewa bao la kuotea,” alidai Aussems.

Kauli ya Aussems inaendana na ukweli wa rekodi ya Al Ahly katika mechi tatu za mwisho ilizocheza uwanja wa nyumbani katika Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Esperance, Jimma Aba Jifar na AS Vita.

Timu hiyo ilipata penalti tatu na mchezaji mmoja wa timu pinzani alionyeshwa kadi nyekundu.

Aussems hakusita kuonyesha hofu kwa waamuzi wa mechi hiyo na amedai akili yake haiwazi wachezaji wa Al Ahly licha ya kufahamu ubora na udhaifu wao.

“Timu za Misri siku zote zimekuwa zikipata sapoti ya waamuzi. Makocha wanajua jinsi ya kuizuia Al Ahly, lakini jambo muhimu wanatimizaje hilo. Ahly wana mapungufu yao lakini wanabaki kuwa timu bora Afrika.

“Uwingi wa mashabiki wao uwanjani hauwezi kuwa tatizo kwa timu yangu kwa sababu kucheza na timu maarufu kunahamasisha wachezaji,” alisema Aussems.

Simba imekuwa haina rekodi nzuri dhidi ya timu kutoka Misri au ukanda wa Kaskazini mwa Afrika kwa kuwa katika mara 10 ilizokutana na klabu za huko, imetoka sare moja na kupoteza mechi tisa ndani ya muda wa dakika 90.

Kipigo zaidi ambacho Simba imewahi kukutana nacho ugenini nchini Misri ni kile cha mabao 5-1 ilichopata dhidi ya wapinzani wao Haras Hodood mwaka 2010 wakati matokeo bora zaidi yalikuwa ni kutoka suluhu na Al Masry mwaka jana katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.



Chanzo: mwananchi.co.tz